Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBS yateketeza vipodozi vya mil 125/

523f669ee30c8b64697858d2dbc2ae5d TBS yateketeza vipodozi vya mil 125/

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza vipodozi vyenye viambata sumu vyenye thamani ya Sh milioni 125 baada ya kufanyika ukaguzi wa kushitukiza kwenye maghala ya kuhifadhia vipodozi ambayo hayajasajiliwa.

Vipodozi hivyo vilivyopigwa marufuku vilikutwa katika maghala la Kampuni ya Kimario Cosmetics na wakaguzi wa TBS jijini Arusha na kukamatwa kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2019.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Roida Andusamile ilieleza kuwa mmiliki wa ghala hilo, Pamphil Kimario amelipa Sh milioni 3.5 ikiwa ni gharama ya kuteketeza bidhaa hizo hatarishi kwa afya ya binadamu kwani zinapotumiwa huweza kusababisha madhara mbambali kwa mtumiaji.

Baadhi wa Watanzania wamekuwa wakitumia vipodozi hivyo vyenye viambata vya sumu ambavyo vina kemikali ya Mercury na Hydroquinone kwa lengo la kung’arisha ngozi zao na hata kubadili rangi ya ngozi hizo bila kujali madhara yatokanayo na bidhaa hizo.

Vipodozi vyenye kemikali ya Mercury kwa Mujibu ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2020, vikitumika kwa muda mrefu vinasababisha magonjwa ya figo, mapafu, ngozi, macho, mfumo wa fahamu, mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na mfumo wa kinga ya mwili na kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ya hydroquinone husababisha magonjwa ya kansa ya ngozi.

Sheria ya Fedha Na. 8 ya mwaka 2019 iliipa mamlaka TBS ya kusimamia usajili wa bidhaa za chakula, vipodozi, maghala ya kuhifadhia chakula na vipodozi pamoja na migahawa na mahoteli jukumu lillilokuwa likifanywa hapo awali na iliyokuwa Mamlaka ya Dawa Chakula na Vipodozi (TFDA).

Utekelezaji wa Sheria hiyo ya Fedha ulianza rasmi Julai 2019, hivyo kuwalazimu wauzaji wazalishaji na wauzaji wa vipodozi kusajili bidhaa hizo pamoja na maghala ya kuhifadhia.

Andusamile alisema shirika pia limeteketeza bidhaa nyingine zisizofaa za vipodozi na vyakula zilizokamatwa katika ukaguzi uliofanyika nyakati tofauti katika maeneo mengine Arusha na nje ya Arusha katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2020.

“TBS inaendelea na ukaguzi huu nchi nzima pamoja na kuwahimiza wazalishaji na wauzaji wa vipodozi kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zilizopo kwa kusajili bidhaa hizo pamoja na maghala li kuepuka usumbufu,”alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz