Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBS yafunda watumishi wa umma kuepuka vipodozi hatari

529e92b2184e21a35ffee0feae600d2b.png TBS yafunda watumishi wa umma kuepuka vipodozi hatari

Tue, 8 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATUMISHI wa umma katika taasisi mbalimbali mkoani Ruvuma wameanza kupata elimu kuhusu madhara ya matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu.

Elimu waliyopewa itawawezesha kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii na familia zao kwa ujumla.

Elimu hiyo ilianza kutolewa kuanzia Mei 31, mwaka huu ikilenga taasisi saba za umma ikiwa ni mwendeleza wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutoa elimu kwa umma kuhusiana na madhara ya vipodozi vyenye viambata vya sumu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na elimu hiyo, Meneja wa TBS Kanda ya Kusini, Amina Yasini alisema wameona watoe elimu kwa watumishi wa umma kwa sababu wanatambua muda mwingi wanakuwa na majukumu hivyo inawezekana hawasikilizi vipindi vya redio vya shirika hilo vyenye kulenga kufundisha umma kuhusiana na vipodozi.

Alisema moja ya majukumu ya TBS ni kudhibiti vipodozi ambavyo vina viambata vya sumu lengo likiwa ni kulinda afya za watumiaji.

Alifafanua kwamba Tanzania imepakana na nchi nyingi, ambako kuna mipaka mingi iliyo rasmi na isiyo rasmi hivyo bidhaa nyingi zinaingia nchini.

"Kwa hiyo shirika letu lina jukumu la kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini ni salama kwa matumizi ya binadamu," alisema na kuongeza:

"Tuna utaratibu wa kupita kwenye masoko kuangalia bidhaa na tukikuta bidhaa ambazo tuna mashaka nazo tunazipima na tukibaini zina viambata sumu tunazikamata na kuziondoa sokoni."

Kwa mujibu wa Yasini shirika haliwezi kushinda vita hiyo wakifanyakazi pekee, ndiyo maana wamekuwa wakitoa elimu hiyo kwenye shule na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.

Alitaja madhara makubwa ambayo mtu anaweza kupata kwenye ni kuwashwa, kuvimba, kuchanikachanika na wakati mwingine kupata kansa ya ngozi.

"Lakini kipodozi kinaweza kikaenda ndani kikaathiri viungo vya ndani, mfano maini, figo na wakati mwingine baadhi ya kemikali zinaweza zikaenda hadi kwenye mfumo wa uzazi kwa hiyo hayo madhara yanaenda hadi kwa watoto, matokeo yake unakuta akizaliwa viungo vyake vinashindwa kujitengeneza vizuri," alisema.

Alisema kupitia elimu hiyo watumishi hao waliweza kuoneshwa aina mbalimbali za vipodozi vyenye viambata vya sumu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz