Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBA yapewa siku 90 kukamilisha hospitali Geita

67261 Tbapic

Thu, 18 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa muda wa siku 90 kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Ujenzi wa hospitali hiyo unaogharimu zaidi ya Sh5.9 bilioni ulianza mwaka 2017 na ulipaswa kukamilika Machi mwaka 2018 lakini haujakamilika hadi sasa.

Akizungumza mjini Geita leo Jumatano Julai 16, 2019 mara baada ya kukagua mradi huo, Waziri Ummy alimtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi huo kuhakikisha kazi inakamilika ifikapo Oktoba, 2019.

“Serikali imeshatoa fedha zote zinazohitajika na tunataka ujenzi ukamilike ili huduma zianze kutolewa kuanzia Disemba Mosi, 2019,” amesema Waziri Ummy

Kaimu meneja mradi wa TBA, Gladys Jefta amemuahidi waziri kuwa mradi huo utakamilika kabla au ifikapo Novemba mwaka 2019 huku akitaja tatizo la umeme, maji na kuchelewa kutolewa kwa fedha ni baadhi ya sababu zilizosababisha uchelewe kukamilika kwa wakati.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy aliuagiza uongozi wa mkoa wa Geita kutumia zaidi ya Sh2.2 bilioni za mfuko wa maendeleo wa Kimataifa (Global fund) kukuamilisha ujenzi wa wodi ya wazazi na wagongwa wa kawaida pamoja na maabara.

Pia Soma

Waziri huyo pia amemwagiza mganga mfawidhi hospitali ya mkoa wa Geita kuanza mchakato wa kuomba watumishi na wataalam kukidhi mahitaji hospitali ya rufaa itakapoanza kufanya kazi.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Dk Japhet Simeo amesema mkoa huo unakabiliwa na upungufu wa watumishi 2, 030, sawa na asilimia 54 ya watumishi 3, 783 wanaohitajika. Watumishi waliopo kwa sasa ni 1, 753, sawa na asilimia 46 ya mahitaji.

Mkoa wa Geita inayokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni mbili kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inatekeleza mpango kabambe wa maboresho ya sekta ya afya kwa kujenga zahanati 300.

Hadi kufikia Desemba 31, mwaka 2019, zaidi ya zahanati mpya 100 zinatarajiwa kuanza kutoa huduma.

Chanzo: mwananchi.co.tz