Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TASAF waimarisha Kituo Cha Afya Nyabilezi

12fd54c07931d2f7e4c5d6a9cdf6bbe2 TASAF waimarisha Kituo Cha Afya Nyabilezi

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wa Kijiji cha Nyabilezi na maeneo ya jirani wilayani Chato watanufaika na huduma za afya zitakazotolewa katika Kituo cha afya cha Nyabilezi baada Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuchangia kiasi cha Sh milioni 569 kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni mstaafu George Mkuchika alisema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na TASAF kitakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya.

Kutokana na umuhimu wa kituo hicho, Mkuchika aliwahimiza viongozi wilayani Chato kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya ifikapo Machi 30, 2021 kama ilivyopangwa ili wananchi wapate huduma ya afya inayostahili.

Waziri Mkuchika aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Nyabilezi kwa kutoa mchango wa fedha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa kuchota maji, kusomba mchanga, kokoto na mawe.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati Medard Kalemani aliishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia TASAF kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kikikamilika kitakuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya katika Kijiji cha Nyabilezi na maeneo jirani.

Pamoja na pongezi hizo, Waziri Kalemani alimuomba Mkuchika kupitia TASAF kujenga kituo kingine cha afya katika Kijiji cha Makurugusi ili kupunguza msongamano wa wananchi watakaofuata huduma za afya katika Kituo cha Nyabilezi.

Awali, Kituo cha Afya cha Nyabilezi kata ya Bukome kilikuwa ni Zahanati, hivyo kutokana na umuhimu wa huduma za afya katika kata hiyo, TASAF imetoa kiasi cha fedha cha Sh milioni 569 ili kukidhi uhitaji wa huduma za afya.

Chanzo: habarileo.co.tz