Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza (TANCDA) na Chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mradi wa RECAP unaosimamiwa pia na shirika la afya Duniani umeandaa mkutano wa usambazaji wa muhtasari wa sera juu ya lishe bora na kushughulisha mwili.
Lengo Ia mkutano huo ni kusambaza muhtasari za kisera zinazolenga kukinga na kupambana na wimbi la magonjwa yasiyoambukiza nchini kwa wahariri wa vyombo vya habari, vyuo na taasisi zisizo za kiserikali huku ikielezwa muhtarsari za kisera ziko mbili kwa ajili ya kushughulisha mwili na ulaji unaofaa.
Aidha wadau wengine walioshiriki mkutano huo uliofanyika jan Februari 21,2022 jijini Dar es Salaam ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wawakilishi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.Wabunge hao ni wale wanaotoka kwenye kamati ya Huduma za Jamii na Kamati ya UKIMWI na Magonjywa yasiyoambukizwa ambao wameshajengewa uwezo kuhusu masuala ya magonjwa hayo na visababishi vyake.
Moja ya mjadala ambao umejadiliwa na washiriki wengi wa mkutano huo ni matumizi ya tumbaku nchini ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani( WHO) kutaka mtumizi ya tumbaku duniani yasiwepo huku mkakati wa Wizara ya Afya upande wa Tanzania Bara na Visiwani wakiwa na muelekeo wa kuangalia nini kifanyike kuhakikisha matumizi ya tumbaku yanaendelea kupungua nchini.
Kwa mujibu wa maofisa wa Wizara ya Afya wamesema kuwa sababu za kuwepo mkakati wa kupunguza utumiaji wa tumbaku unatokana na ukweli kwamba tumbako ni moja ya kisababishi kikubwa cha magonjwa yasiyoyakuambukiza nchini,hivyo njia mojawapo ya kukabiliana na magonjwa hayo ni kupunguza matumizi ya tumbaku.
Baada ya kuelezwa hivyo baadhi ya washiriki wameunga mkono kupunguzwa kwa matumizi ya tumbaku lakini wengine wameonesha kutokuwa tayari kupunguzwa kwa matumizi ya tumbaku kwa kuzingatia kuna wakulima wanategemea zao hilo kupata fedha lakini Serikali nayo imekuwa ikipata mapato.
Akizungumza mbele ya washiriki wa mkutano huo Meneja wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bakari Magarawa amesema kwa Zanzibar wamekuwa na mikakati mbalimbali ikiwemo ya kutoa elimu itakayosaidia jamii kuachana na matumizi ya tumbaku Kama njia mojawapo ya kukabiliana na magonjwa yasiyoyakuambukiza.
"Kwa Zanzibar magonjwa yasiyoyakuambukiza ni changamoto kubwa na hii inatokana na sababu mbalimbali ukiwemo ya mtindo wa maisha,matumizi makubwa ya kemikali katika vyakula, kutofanya mazoezi .Lakini tumbaku imekuwa chanzo kikubwa cha magonjwa hayo hasa saratani.Tumbaku inasababisha saratani kwa kiwango nchini kwetu lakini hata wenzetu wa Shirika la Afya Duniani ( WHO) imekuja na mpango wa kuondoa kabisa matumizi ya tumbaku.
"Kwa hapa kwetu hatuwezi kusema kuanzia leo matumizi ya tumbaku hapana,hatutaeleweka ,hivyo tunaamini tukitoa elimu ya kutosha tutaanza kupunguza kidogo kidogo matumizi ya tumbaku ,tunajua kuna mikoa inalima tumbaku lakini kinachoweza kufanyika ni kutafuta mazao mbadala ambayo wakulima watalima.Ukiangalia faifa inayopatikana kutoka kwenye tumbaku ni ndogo ukilinganisha madhara,"amesema Magarawa.
Kwa upande wake Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Pwani Hawa Mchafu Chakoma amesema kuna haja ya Wizara ya Afya pamoja na wadau kuendelea kuweka mikakati itakayosaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambikiza huku akitoa pongezi kwa TANCDA kwa uamuzi wake wa kushirikisha vyombo vya habari katika mkutano huo kwani ni wadau muhimu.
Akizungumza tumbaku amesema inaleta magonjwa yasiyoyakuambukiza lakini Serikali inapata mapato , Wizara ya Viwanda na Biashara wenyewe wanahamasisha,hivyo uwepo wa waandishi wa habari utasaidia katika kupaza sauti na kuieleza jamii kuhusu madhara.
Pia ametoa ombi kwa Wizara ya Afya kuweka mipango madhubuti katika kukabiliana na magonjwa hayo huku akieleza kwa sehemu kubwa wamekuwa wakijikita katika miradi bila kuifanyia tathimini kujua kama miradi hiyo imefanikiwa au laa.
Wakati huo huo baadhi ya waandishi wametoa ombi kwa wadau kuweka mikakati itakayosaidia kukabiliana na magonjwa na vyombo vya habari viko tayari kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha inakuwa na uelewa wa kujiepushana na magonjwa hayo kwa kubadilisha mitindo ya maisha.
Kwa upande wake Dk.Anzibert Rugakingira kutoka Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza Wizara ya Afya amesema mpango huo ulianzishwa mwaka 2019 chini ya Wizara ya Afya. Lengo kuu likiwa ni uratibu wa afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ndani na nje ya Sekta ya Afya.
"Sambamba na Mikakati ya Sekta ya Afya, Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza pia hutekeleza afua zilizobainishwa kwenye Sekta nyingine mtambuka kama vile Elimu, Kilimo, Michezo, Viwanda, Biashara, Maji nk."