Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAMISEMI yaagiza upimaji vinasaba vya Selimundu kabla ya ndoa

Sickle Cell Red Cells Blood Upimaji vinasaba vya Selimundu

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Afya), Dk Grace Maghembe ameagiza elimu juu ya umuhimu wa kupima vinasaba vya ugonjwa wa selimundu ifundishwe shuleni na vyuoni, ili kupunguza watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo.

Alitoa kauli hiyo jana, alipozungumza na wadau wa kampeni ya vunja mduara iliyoandaliwa na Mtandao wa Asasi unaopambana na ugonjwa wa selimundu (Tanscda).

“Tufundishe shuleni, vyuoni na viongozi wa dini tuwashirikishe ili waelimishe waumini umuhimu wa kupima vinasaba kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa, ili kupunguza watoto wenye changamoto ya selimundu,”alisema.

Mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, Dk Deogratias Soka alisema lengo la kukutana kwao ni kutoa ripoti ya utekelezaji wa kampeni hiyo iliyofanyika mikoa 13 nchini.

Advertisement Alisema kampeni hiyo inalenga kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu nchini ambapo takwimu zinaonyesha watoto 11,000 wanazaliwa kila mwaka na ugonjwa huo.

Alitaja mikoa mitano ya kanda ya ziwa inayoongoza kwa kuwa na watu wengi wenye vinasaba vya ugonjwa huo, ukiwemo Mkoa wa Kagera ambao una asilimia 22.99.

Mikoa mingine inayoongoza ni Mwanza (21.11), Mara (21.10), Shinyanga (19.90) na Geita (16.96).

Dk Soka alisema Tanzania ni nchi ya nne kwa kuwa na wagonjwa wa selimundu wengi duniani, ikizifuatia nchi za India, Nigeria na Congo.

Alisema ugonjwa huo umekuwa unachangia vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano kwa asilimia saba, yaani vifo vinne kwa kila vifo 1,000 vinatokana na ugonjwa huo.

“Tuliona tuje na huu mpango wa kupunguza vifo vya selimundu kwa kutoa elimu. Cha muhimu ni namna gani tunaweza kupunguza tatizo la selimundu ama kujikinga. Sehemu ya pili ni kuwapima pia kugundua kama wana vinasaba vya ugonjwa huu,” alisema.

Alisema asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania, sawa na zaidi ya watu milioni tano wanakadiriwa kuwa na vinasaba vya ugonjwa huo.

Alisema katika kampeni hiyo iliyozinduliwa Machi 29 mwaka 2019, vyuo sita na shule za sekondari 32 walifikiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live