Watu watatu wamepoteza maisha na wengine 316 wameugua ugonjwa wa surua Visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kitengo cha Elimu ya Afya wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Bakar Magarawa mlipuko wa ugonjwa huo umetokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Agosti 26, 2022 wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Internews kuhusu namna ya kuandika habari za Covid-19 mjini hapa.
"Leo asubuhi tumepewa taarifa bado idadi inaendelea kupanda na Wilaya zote 11 za Zanzibar zimeripotiwa kuwa na wagonjwa hao isipokuwa Wilaya ya Wete huku Wilaya ya Mjini Magharibi ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi ya 200," amesema.
Amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao kuwachanja kwenye vituo vya afya huku akitaja umri unaoathirika zaidi ni miaka mitano kushuka chini licha ya wagonjwa hao walioripotiwa kuwamo na wenye umri wa miaka 15 kushuka chini.
"Watoto wetu jamani tuwapeleke wachanje waende kwenye vituo vya afya, tumeweka chanzo hizi ni bure," amesema.
Chanjo ya surua hutolewa kuanzia watoto wa miezi tisa na hurudiwa baada ya mtoto kufikisha mwaka mmoja na nusu.
Kwa mara ya kwanza, taarifa za ugonjwa huo zilitolewa na Waziri wa Afya kisiwani humo, Nassor Mazrui Agosti 9, 2022 ambapo kwa wakati huo walikuwa wameripotiwa wagonjwa wagonjwa 80.
Surua ni moja ya magonjwa ya kuambukizwa ambayo husababishwa na virusi aina ya morbillivurus paramyxvirus vinavyoenea kwa haraka kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa au kugusa majimaji yatokanayo na mwenye maambukizi.