Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sumu kuvu inasababisha saratani, inashusha CD4

92333c191370506eb0bfb18d0a7c990b Sumu kuvu inasababisha saratani, inashusha CD4

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SUMU kuvu ni aina ya kemikali za sumu zinazozalishwa na ukungu au fangasi wanaoota kwenye mbegu za nafaka yakiwemo mahindi, mbegu za mafuta kama vile karanga, jamii ya kunde, mazao ya mizizi na pia vyakula na malisho ya wanyama.

Kwa mujibu wa Jarida la Mkulima Mbunifu, sumu hiyo inajulikana kitaalamu kwa jina la mycotoxins.

Jarida hilo linabainisha kwamba, sumu kuvu pia hupatikana katika mazao ya mifugo kama vile maziwa, mayai na nyama pale ambapo chakula kinacholiwa na mifugo kitakuwa kimechafuliwa na sumu hizo.

Vilevile baadhi ya sumu kuvu hupatikana kwenye maziwa ya mama anayenyonyesha iwapo atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hizo.

Ingawa kuna aina nyingi za fangasi wanaoweza kuota na kukua katika vyakula hivyo, ni wachache tu wanaotoa sumu kuvu. Sumu kuvu haiwezi kuonekana kwa macho, haina harufu, haina kionjo na wala haina rangi.

Ukungu unaotokana na sumu kuvu unaweza kuwa na rangi ya kijani, chungwa, kijivu, au njano chafu na unaweza kutoa harufu ya uvundo.

Ukungu unaotoa sumu kuvu hustawi ikiwa mazao yamekumbwa na ukame yakiwa shambani au kushambuliwa na wadudu waharibifu na yakahifadhiwa kwenye ghala lenye joto na unyevu wa kiwango cha juu.

Vyakula vinavyoweza kuambukizwa sumu kuvu ni kama vile mahindi na unga wake, karanga na mazao yanayotokana na karanga, muhogo, nyama, mayai na maziwa (vyakula vitokanavyo na mnyama au ndege aliyeambukizwa pamoja na mazao yao) na vyakula vya mifugo vyenye mbegu zilizoambukizwa au nyasi au vyakula vya mifugo vya kutengenezwa.

Binadamu au mnyama anaweza kula sumu kuvu kupitia vyakula vinavyochafuliwa na ataathiriwa kutegemeana na kiasi cha sumu kuvu kilichomo.

Tafiti nyingi za kisayansi zimeonesha uhusiano wa sumu kuvu na athari mbalimbali za kiafya kama vile saratani hasa ya ini, kushusha kinga ya mwili, kudumaa hasa kwa watoto.

Sumu hiyo pia inaweza kuathiri figo, inasababisha vifo kwa binadamu na wanyama ikiwa viwango vya sumu hiyo ni vikubwa. Baadhi ya sumu kuvu hutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa bado tumboni.

Athari za kiafya zinaweza kujitokeza baada ya muda mrefu wa matumizi. Sumu inaweza kujikusanya na kuendelea kuwa nyingi mwilini kidogo kidogo kulingana na mtu atakavyokuwa anaendelea kula vyakula vilivyo na sumu hiyo.

Mbali na madhara ya kiafya, uchafuzi wa sumu kuvu huathiri pia uhakika wa chakula na biashara.

Mazao ya kilimo yakikutwa na sumu kuvu iliyozidi kiwango kinachokubaliwa hayakubaliwi kwenye masoko ya nje ya nchi na badala yake yanateketezwa.

Kuna njia mbalimbali ambazo mkulima anaweza kuzitumia ili kupunguza uchafuzi wa sumu kuvu katika mazao yakiwa shambani au baada ya kuvuna.

Njia hizo ni kama zifuatazo;

• Lima aina za mazao yenye ukinzani dhidi ya kuvu wanaotoa sumu kuvu.

• Vuna mazao yakiwa yamekauka vizuri kama inavyoshauriwa na Ofisa Kilimo na pia epuka kuyaharibu mazao yako.

• Usianike mazao kwenye udongo. Tumia turubai au aina nyingine ya vifaa vya kuanikia au kukaushia mazao

• Wakati na baada ya kuvuna chambua na kuondoa mbegu zilizooza, zilizovunjika, zilizotobolewa au kuharibiwa na wadudu na zile zilizobadilika rangi.

• Hifadhi mazao mahali pakavu na pasipo na joto. Hakikisha mazao yaliyohifadhiwa hayanyeshewi na mvua au kuloa maji.

• Hifadhi mazao kwenye ghala linaloruhusu mzunguko wa hewa.

• Zuia wadudu waharibifu na kuvu kwa kunyunyiza madawa yaliyokubalika na kushauriwa na wataalamu wa kilimo.

• Unaweza pia ukakoboa mahindi na kuchambua vizuri kabla kuyahifadhi ili kuondoa yale yanayoelekea kuwa na uchafuzi wa sumu kuvu ambayo huwa zimeanza kubadili rangi.

• Tumia dawa ya kibayolojia kama vile Aflasafe (aina ya kuvu ambaye hukinzana na yule anayetoa sumu kuvu).

• Tumia dawa iliyothibitishwa kuondoa sumu kuvu.

Chanzo: habarileo.co.tz