Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika masikioni janga kwa vijana-Utafiti

C8d73cd57301068201bd04d8fb673407 Spika masikioni janga kwa vijana-Utafiti

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UTAFITI wa wataalamu umebainisha matumizi ya muda mrefu ya spika za masikioni ni janga huku vijana wakitajwa kuwa ni waathirika wakubwa watakaopoteza uwezo kusikia kutokana na matumizi ya muda mrefu ya vifaa hivyo.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia na cha Bergen cha Norway ndiyo wamebainisha hayo kupitia mradi wa pamoja (Norhed) wa utafiti wa athari za Kelele kwa Usikivu wa Binadamu Mahala pa kazi.

Mtafiti kutoka Muhas, Dk Israel Nyarubela , alitoa taarifa juu ya utafiti huo hivi karibuni mjini Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),baada ya makamu mkuu wa Chuo kikuu hicho kufungua kikao cha utoaji taarifa ya ushirikiano wao na vyuo hivyo vya nje.

Alisema kitu ambacho kinapaswa kifahamike ni kuwa madhara ya kelele kwenye usikivu hayatokei mara moja bali huwa ni ya taratibu kwa sababu yanaathiri sehemu ya ndani ya sikio hivyo usikivu huendelea kupungua taratibu.

“Utafiti unaonesha earphone na headphone si salama sana kutumia kwa muda mrefu… changamoto ni vya starehe kila mtu anataka kupata ladha ya muziki au kitu kingine anachokisikiliza…hivyo kudhibiti kiwango salama cha sauti ambacho hakiwezi kuleta madhara kwa masikio ni changamoto kubwa sana. “

Alisema kwa matumizi ya vifaa hivyo , utafiti umeonesha kuwa imekuwa ni janga hususani kwa vijana kwani linawakumba kwa wingi na kwamba uwezekano wao wa kusikia unapungua taratibu.

“Najua ya kwamba kuna kiwango ambacho kimewekwa hapa nchini na TBS ambacho si salama sauti ikizidi desibeli 85 hapo inaweza kuleta madhara “ alisema Dk Nyarubela.

Dk Nyarubela , alisema: “Natukumbuke ukiingia kwenye klabu kwa mfano unapoingia utasikia kelele kubwa sana inaleta karaha lakini baada ya muda utakuwa kawaida mwili utakuwa umefanya kazi yake ya kuizoea hali hiyo , lakini ukumbuke hakuna kilichobadilika sauti ni kubwa vile vile na unapoendelea kuishi kwenye mazingira hayo unaanza kuathiri usikivu wako.”

Alisema kuwa tafiti nyingi zimefanyika na kuonesha vifaa hivyo vina madhara kwa wasikilizaji ( watumiaji) . Alisema watu wengi hasa vijana wameiona imekuwa ni mfariji na mwenza wao wanapokuwa katika safari ,kupumzika na shughuli nyingine wakati madhara yake ni makubwa kwa siku zijazo.

“Tunashauri lazima mtu aelewe hivyo sio mbaya ila usishawishiwe na huo muziki , kwani ni kishawishi kwa maana unashawishika kuongeza sauti bila kujua kuwa kesho na kesho kutwa, usikivu wako unapungua ,“ alisema Dk Nyarubela.

Dk Nyarubela, alisema kwenye matamasha yanayofanyika wanamuziki wengi wa nje ya nchi wamefanyiwa tafiti hizi na wakagudulika kuwa wanashida na usikivu.

Hata hivyo , alisema katika nchi zilizoendelea, wanamuziki wengi wanavaa spika maalumu zenye kifaa cha kurekebisha sauti na siyo sauti iliyopo ukumbini . Hii ni baada ya kubainika wanamuziki wengi wa zamani waliathirika kupitia vyombo vya muziki kwa sababu ya mlio mkubwa wa sauti.

“Kwa sasa wamekuja na taaluma mpya na unaweza kuwaona wanamuziki wamevaa hizo headphone na watu wengine wakadhani ni fasheni , sio bali wataalamu wamepima sikio lake,” alisema Dk Nyarubela.

Alisema kupitia tafiti zilizofanyika, Muhas kimeweza kupata vifaa vya kisasa vya kufundishia . Alisema hivi karibuni wamepatiwa kifaa cha kisasa cha kupima kiwango cha usikivu kwa wafanyakazi mahala pa kazi.

Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Andrew Pembe, katika hotuba yake ya ufunguzi alisema licha ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kasi ni kubwa , ni wajibu sehemu za kazi na viwandani kuwa salama zaidi kwa wafanyakazi .

Profesa Pembe, alisema maeneo hayo ya viwanda yanahitajika kuboreshwa , kuangaliwa kwa karibu afya za watu zisidhurike kutokana na shughuli za viwandani .

“ Usalama zaidi kwenye eneo hilo tutakuwa tumechangia zaidi kwenye lengo kuu la taifa hili kwenda kwenye uchumi wa viwanda na wananchi wa Tanzania wakiwa na afya njema “ alisema .

Profesa Pemba alisema ushirikiano umenufaisha chuo chao kwa kupatiwa kifaa cha kisasa cha kupima sauti katika masikio kubaini wanaopata matatizo ya sikio kutokana na kelele za kwenye viwanda wakati wa uzalishaji.

Chanzo: habarileo.co.tz