Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Soma hapa maajabu ya panya kurahisisha tafti za TB

Panya TB Soma hapa maajabu ya panya kurahisisha tafti za TB

Wed, 1 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefuga Panya Buku zaidi ya 90 wenye uwezo wa kubaini vimelea vya Kifua Kikuu (TB) kutoka kwenye sampuli 100 kwa dakika nane.

Akizungumza leo katika kongamano la miaka 60 lilioandaliwa na SUA na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwalimu wa Panya hao, Mariam Chamkwata amesema sampuli hizo zinachukuliwa kutoka kwenye makohozi ya binadamu anayetakiwa kupimwa.

Chamkwata amesema panya hao pia wanatumika kunusa mabomu yaliyotegwa ardhini kwa kutumia dakika zisizozidi mbili huku ikielezwa kwamba matumizi ya viumbe hao yanahimizwa kutokana na urahisi wao kupita katika sehemu hatarishi.

"Tunashirikiana na taasisi za afya nchini kutambua vimelea vinavyosababisha maambukizi ya TB kwa kutumia panya hawa, pia tunawafundisha mbinu za kunusa harufu ya sehemu zilizotegwa mabomu ya ardhini," amesema Chamkweta

Meneja mradi wa kupima kifua kikuu kwa kutumia panya buku Tanzania, Dk Joseph Soka amesema matumizi ya panya hao yamesaidia kubaini vimelea vya kifua kikuu kwa wagonjwa ambavyo havikutambulika kwa urahisi kupitia vifaa.

"Kuna wakati maambukizi ya vimelea vya TB vinaweza visitambulike kwa urahisi kupitia mitambo ya kitaalam, lakini endapo panya huyu akisema sampuli ina vimelea vya TB inatusaidia kubaini maambukizi ya ugonjwa huo kwa binadamu kwa urahisi," amesema Dk Soka

Dk Soka amewataka wananchi kujitokeza kupima maambukizi ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa kwa kutumia panya buku hao kwani iwapo mtu mwenye maambukizi asipotibiwa kwa wakati anaweza kuambukiza vimelea hivyo kwa watu hadi 20 ndani ya mwaka mmoja.

Mshiriki katika kongamano hilo, John Samweli amesema hakutarajia kuona jamii ya wanyama hao ikitumika kurahisisha tiba kwa binadamu huku akitoa wito kwa chuo hicho kufuga panya zaidi ili kurahisisha kubaini uginjwa huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live