Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahamu wanawake Mkahara kutoshika ujauzito

Mimba AB Sintofahamu wanawake Mkahara kutoshika ujauzito

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wanawake wanaoishi katika kijiji cha Mkahara Halmashauri ya mji Nanyamba mkoani Mtwara wameiomba Wizara ya Afya kuwaletea watalaamu katika kijiji chao ili kuweza kuwasadia kujua tatizo linalopekelea kutobeba ujauzito.

Wanawake hao wanakadiriwa kuwa ni zaidi ya 40 ambapo wamezungumza na Mwananchi na kutoa kilio chao huku wakiiomba serikali iwasaidie.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 11,2023 kijijini hapo, Zainabu Hassan amesema kuwa ameishi kwenye ndoa zaidi ya miaka 10 hajawahi kushika ujauzito hali ambayo inaiweka ndoa yake matatani.

Amesema kuwa serikali imekuwa ikiboresha huduma za afya tunaomba nasisi zitufikie ili tuweze kupata tiba na sisi tubebe watoto wetu.

“Shida yangu kubwa ni kuzaa sijazaa mtoto hata mmoja niko kwenye ndoa zaidi ya miaka 10 hadi mume wangu ameamua kuoa mke mwingine na tayari ameshazaa, inaumiza na inatutesa sana tunaomba wizara ya afya ituletee watalaamu watuangalie na watusaidie,” amesema na kuongeza.

“Haijalishi tutasubiri kwa muda gani tunahitaji watoto yaani nimeachika ndoa nne naachwa kwasababu sizai nimebakia natanga tanga pesa imekuwa tatizo matibabu makubwa ni pesa,” amesema.

Naye Abdallah Hamis (mume wa Zainabu) amesema kuwa alioa miaka 10 iliyopita ambapo licha ya mkewe kuwa na afya njema lakini hajawahi kupata ujauzito.

“Tumejaribu kwenda katika maeneo mbalimbali hospitalini lakini hatujafanikiwa tumeenda mpaka kwa waganga wa kienyeji lakini hatukupata suluhu,”

Mwenyekiti wa kijiji cha Mkahara, Ismail Mkanyanga amesema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakitoa taarifa kwake wakiomba wapate msaada wa watalaamu wa masuala ya uzazi.

“Nikweli tunao watoto wachache sana, hata shule yetu ya msingi kuanzia awali hadi darasa la saba kuna watoto 195 tu ambapo darasa lenye watoto wengi hawafiki 28 na lenye wachache wako 15 tu tunaomba Serikali ya wawasaidie wakina mama hawa,” amesema Makanyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda amesema kuwa suala la kutoshika ujauzito kwa mwanamke ni suala pana ni vema watalaam wakafika na kufanya uchunguzi.

“Nimepokea taarifa kuwa kuna wanawake wanachangamoto ya kupata watoto lakini nao wameenda mbali sana na kuita kuwa ni ugumba, siwezi kusema ipo lakini nitaelekeza watalaam wa afya waweze kufika wafanye utafiti na vipimo ili kudhibitisha uwepo wa hali hiyo,”

“Ni vema wanawake wakatambua kuwa wanapohisi dalili ambayo sio sawa kwenye mwili wao wanapaswa waenda vituo vya afya wakati mwingine tunatumia vitu mbalimbali vivavyoweza kuleta athari kwenye mwili wa mwanamke bila kufahamu,” amesema.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji Nanyamba, Dk Dickson Masare amesema kuwa amepokea maombi hayo na atayafanyia kazi kwa kuweka utaratibu ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo kwake limefika kwa mara ya kwanza.

"Wanawake wengi wanatumia uzazi wa mpango hizo nazo zinaweza kuwa sababu kubwa ya kuwafanya baadhi ya wanawake kutopata haraka ujauzito, wapo wanaoweka za miaka mitano ambayo huenda mpaka miaka saba ikiwa haijaisha nguvu.

Wengine wanakuwa na uvimbe ambao unapekelea kushindwa kupata ujauzito hivyo tutakutana nao na kufanya vipimo ili tuweze kuwasaidia,” amesema Dk Masare.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live