Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku ya mtoto wa Afrika: Athari za virusi vya Corona kwa watoto

508f160cd2a8c889.jpeg Siku ya mtoto wa Afrika: Athari za virusi vya Corona kwa watoto

Thu, 17 Jun 2021 Chanzo: kiswahili.tuko.co.ke

Mwaka 1991, Jumuiya ya Nchi Huru za Afrika (AOU) ambayo sasa inajulikana kama Umoja wa Afrika (AO), ilitangaza Juni 16 kila mwaka kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika.

Hii ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya Soweto, nchini Afrika Kusini Juni 16, 1976 ambapo polisi waliwashambulia kwa risasi wanafunzi waliokuwa wakiandamana.

Walikuwa wakipinga mfumo na elimu duni waliokuwa wanapatiwa, na pia waliitaka serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini kuboresha mfumo wa lugha ya kufundishia.

Mwaka huu, kaulimbiu ya Siku hii ni “Tutekeleze Ajenda 2040: Kwa Afrika Inayolinda Haki za Mtoto”.

Kauli mbiu hii inaonyesha nia dhahiri ya kulinda haki za mtoto katika bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya kulindwa, haki ya kuendelezwa elimu, haki ya kushiriki na haki ya kutobaguliwa.

Katika makala hii nitazungumzia athari za janga la virusi vya Corona kwa watoto, hususan katika kutimiza haki za mtoto.

Baada ya janga hili kutokea, nchi nyingi zikiwemo za Afrika zilifunga shughuli zote za kijamii: shule zilifungwa, biashara zilifungwa, na watu walishauriwa kukaa majumbani ili kuweza kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Katika nchi kadhaa duniani, ripoti zinaeleza kuwa wakati wa janga la virusi vya Corona, watoto wengi wa kike walipata ujauzito ama kuingia katika ndoa za utotoni, na hivyo kukatisha mustakbali wa wengi wao kielimu hata pindi shule zitakapofunguliwa.

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa Novemba mwaka jana, ilionya kuwepo kwa ongezeko kubwa la madhara ya janga la virusi vya Corona kwa watoto.

Nchini Tanzania, wakati shule zilipofungwa kwa miezi mitatu kuanzia Machi mwaka jana, wasichana 101 mkoani Shinyanga waliripotiwa kupata ujauzito na wengine kufungishwa ndoa za utotoni.

Athari kama hiyo si kwamba ilitokea mkoani Shinyanga au nchini Tanzania pekee, nchini Uganda, kwa kipindi cha siku 90, wasichana zaidi ya 1,300 wamepata ujauzito, na ni katika kipindi hiki ambacho shughuli za kijamii ikiwemo shule zimefungwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

Athari nyingine ambayo imewakumba watoto wakati wa janga hili la virusi vya Corona, na kukosa huduma muhimu kwao, ikiwemo utoaji wa chanjo za kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile surua, kifaduro na polio na lishe.

Kutokana na kufungwa kwa shughuli za kijamii, imekuwa vigumu kwa wazazi ama walezi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya kupata chanjo muhimu zinazotakiwa, lakini pia, wahudumu wa afya waliokuwa wakitembelea makazi ya watu kutoa chanjo husika pia wanashindwa kufanya hivyo.

Matokeo yake ni kwamba, watoto wanakuwa hatarini zaidi kupata magonjwa ambayo wangeweza kuyaepuka kama wamgepata chanjo kwa wakati husika.

Katika baadhi ya nchi masikini, watoto wengi walikuwa wakitegemea kupata chakula wakiwa shuleni, lakini kutokana na shule kufungwa, hawakuweza kupata chakula. Ripoti zinaonyesha kuwa, mpaka kufikia mwezi Oktoba mwaka jana, watoto milioni 265 duniani hawakwenda shuleni na hivyo kukosa huduma ya mlo bora

Ulinzi wa watoto, wa kike ama wa kiume, ni jukumu la jamii nzima. Wakati tukiadhimisha Siku hii ya Mtoto wa Afrika, tunapaswa kukumbuka kuwa, watoto wana haki ya kulindwa, wana haki ya kusoma, wana haki ya kucheza.

Tunapaswa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya unyanyasaji na udhalilishaji, na kuhakikisha kuwa, licha ya majanga ya kimaumbile na majanga kama virusi vya Corona, watoto wanaendelea kukua na kuishi maisha yasiyokuwa na shinikizo lolote.

Watoto, wa kike na wa kiume, wanapaswa kulindwa na haki zao kuheshimiwa.

Ni kwa kushirikiana kwa pamoja kati ya wazazi, walezi, waalimu, na serikali, ndipo haki za mtoto zinaweza kutimishwa kithabiti na kuhakikisha mustabali wa maisha yao ya baadaye.

Chanzo: kiswahili.tuko.co.ke