Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Si kweli kwamba katika kila Watanzania wanne mmoja kichaa

21824 AKILI+PIC TanzaniaWeb

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Vijana wanaoishi katika mazingira magumu na yenye machafuko wametajwa kuwa hatarini zaidi kukumbwa na magonjwa ya akili huku Dk Damas Andrea akikanusha madai kwamba katika kila Watanzania wanne, mmoja ana matatizo ya akili.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Oktoba 10, 2018 wakati akitoa tamko la siku ya afya ya akili duniani kwa mwaka 2018.

Katika tamko lililosomwa na mganga mkuu wa Serikali, Mohamed Kambi, amesema kwa Tanzania ukatili na unyanyasaji kwenye mitandao ya kijamii nao unaelekea kuchukua sura mpya na huenda baadaye ikawa sehemu kubwa ya janga linalotishia afya ya akili na ustawi wa vijana.

Kambi amesema takwimu za Shirika la Afya Duania (WHO) zinaonyesha nusu ya wagonjwa wote wa akili huanzia umri wa miaka 14 na wengi wao hawapati nafasi ya kutambulika na kupatiwa matibabu kwa wakati muafaka.

Amesema magonjwa ya akili na matumizi ya vilevi ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya na kiusalama zinazoathiri rika la vijana katika mataifa yote.

Kwa mujibu wa mganga mkuu, ugonjwa wa sonona unashika nafasi ya tatu kwa magonjwa yote yanayoathiri vijana duniani na chanzo kikuu cha pili cha vifo vinavyowakabili vijana duniani.

“Kwa Tanzania mwaka 2015 takwimu zilionyesha vijana wa miaka 13-17 waliomo katika shule za msingi na sekondari katika mikoa 21 ya Tanzania bara zinaonyesha uwepo wa dalili za sonona na kwa zaidi ya asilimia 7 waliohojiwa na asilimia 14 walionyesha kutaka kujiua,” amesema Kambi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Taasisi ya Mirembe, Dk Enock Changalawe amesema magonjwa ya akili mengi hurithiwa kutokana na historia ya familia au ukoo.

 

Hata hivyo, Dk Changalawe amesema wanaume wengi wameonekana kukumbwa zaidi na tatizo hilo kuliko wanawake japo kumekuwa na tatizo la matibabu kwani wengi huchelewa kupata tiba.

Kwa upande wake, Dk Damas alikanusha madai ya kuwa katika kila Watanzania wanne, mmoja ana matatizo ya akili akisema hakuna kitu cha namna hiyo wala utafiti uliothibitisha hilo.

Dk Damas amesema matatizo ya akili huchangiwa na wagonjwa kucheleweshwa kwani zaidi ya asilia 60 hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa baada ya kuanzia kwa waganga wa kienyeji.

Hoja ya kwamba katika kila Watanzania wanne mmoja ana matatizo ya akili au ni kichaa imeenea maeneo mbalimbali nchini jambo ambalo Dk Damas analikanusha kwa madai kwamba halina ukweli wowote.

Chanzo: mwananchi.co.tz