Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shujaa aliyebaini wagonjwa 120 wa TB

Kifua Kikuu.jpeg Shujaa aliyebaini wagonjwa 120 wa TB

Mon, 25 Mar 2024 Chanzo: mwanachidigital

Niliugua Kifua Kikuu (TB) mwaka 2012, nikaanza matibabu nilipopona nikaona kuna watu wengi wanafariki kwa ugonjwa huu kwa kukosa elimu ndiyo maana nikasema sitoruhusu hilo liendelee kutokea.”

Ni kauli ya Grace Kilunguda (62), shujaa aliyejitwika jukumu la kubaini watu wenye dalili za ugonjwa wa TB.

Grace ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kangae Kata ya Nyakato wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, anasema hakutarajia iwapo uvimbe uliomtoka shingoni ungekuwa TB iliyomsotesha kitandani kwa zaidi ya miezi 12.

Huku akiugulia maumivu ya uvimbe huo, Grace amesema alianza kuonyesha dalili za kupungua uzito, kikohozi kikavu na kisichokoma, homa ya mara kwa mara, kutokwa jasho jingi mwilini hasa usiku anapokuwa amelala na baadaye kuanza kutema damu.

Huku akitumia dawa bila kuelekezwa na watalaamu, afya yake ilizidi kutetereka, ndipo familia yake ilimpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure na kuchukuliwa sampuli ya ‘makohozi’ kwa ajili ya uchunguzi, majibu yalibainisha kwamba anasumbuliwa na TB.

“Baada ya kuanza matibabu kwa miezi isiyopungua mitatu nilimaliza dozi yangu na kupona kabisa, baada ya kupona nilirejea nyumbani na kuendelea na kuihudumia familia yangu,” amesema Grace.

Baada ya kukaa na familia yake, Grace amesema alisukumwa kurejesha kwa jamii ndipo alipokwenda katika Ofisi ya Mwitikio wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (Mkuta) wilayani Ilemela, kujengewa uelewa kuhusu ugonjwa wa TB kisha kuanza utambuzi wa watu mwenye dalili za ugonjwa huo.

“Huwa natembelea sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko ya jamii, vilabu vya pombe, makanisa, masoko, tunaenda kuibua watu na kuwaunganisha kwenye Hospitali ya Buzuruga na nyingine. Kwa mfano Machi mwaka huu nimefanikiwa kuibua wagonjwa watano na wamenza matibabu,” amesema.

Mkazi wa Mtaa wa Kangae Kata ya Nyakato wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, Grace Kilunguda (kushoto) ambaye ni shujaa aliyejitwika jukumu la kutoa elimu na kubaini watu wenye dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu(TB). Picha na Mgongo Kaitira

Grace ambaye ni mama wa watoto watatu na wajukuu saba amesema kwa kipindi cha miaka saba ya kufanya kazi ya utambuzi wa watu wenye dalili za TB amefanikiwa kuibua watu wenye TB zaidi ya 120 na kuwaunganisha katika vituo vya afya wakatibiwa hadi kupona.

Amesema uamuzi huo hajawahi kuujutia kwa kuwa hata familia yake inamuunga mkono huku akitaja changamoto anazopitia kuwa ni pamoja na kukosa usafiri wa kumfikisha maeneo yasiyofikika kwa urahisi ili kusaidia kubaini wagonjwa hao.

“Elimu kwa umma kuhusu TB bado haitoshelezi, naomba Serikali itoe elimu ya kutosha hasa maeneo ya ndani zaidi, kuongeza mwamko wa jamii ijitokeze kupima, pia naomba Serikali itusaidie mashujaa, tupate usafiri wa kuzifikia kaya kwa urahisi, tupewe vifaa vikiwemo viatu, glovu na maski.

“Mashujaa tuliogua na kupona TB ambao tumejitolea kutoa elimu kwa umma na kuibua wagonjwa ndani ya jamii, tukiwezeshwa ipasavyo naamini tutaibua watu wengi zaidi wenye dalili za TB, kuwafikisha hospitalini wakatibiwe na hatimaye kutokomeza kabisa ugonjwa huu nchini,” amesema.

Mratibu wa Mkuta Kanda ya Ziwa, Happiness Ogulo ameieleza Mwananchi kuwa Grace ni mmoja kati ya mashujaa 250 wa TB kanda ya ziwa waliojitolea kufanya kazi ya utambuzi wa watu wenye dalili za ugonjwa huo na kuwafikisha katika vituo vya afya kufanyiwa uchunguzi.

Amesema mashujaa hao wamekuwa msaada mkubwa na kurahisisha kazi kwa watalaamu wa afya huku akiwataka mashujaa ambao bado hawajajiunga katika klabu za TB 26 zilizoanzishwa katika kanda hiyo, kujiunga ili kunusuru maisha ya walio hatarini kuugua ugonjwa huo.

“Tunawatumia watu waliotibiwa na kupona akiwamo Grace na wanatusaidia kwa kiasi kikubwa kuwabaini watu ambao wana dalili au wanaumwa TB katika jamii zao. Grace amekuwa mfano wa kuigwa kwetu, amejitolea kujifunza na kuanza kutoa elimu hadi kanisani kuhusu ugonjwa huo,” amesema Ogulo.

Chanzo cha TB

Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukimwi Wilaya ya Ilemela mkoani humo, Dk Rehema Mgallah amesema TB hutokea pale bakteria anayeitwa ‘mycobacterium tuberculosis’ anaposhambulia tishu za mwili ikiwamo mapafu, figo, uti wa mgogongo hata ubongo.

Amesema baada bakteria huyo kuingia na kushambulia eneo la mwili huweza kusambazwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu mwingine hivyo kusababisha maambukizi kusambaa zaidi endapo asipodhibitiwa.

Amesema TB imegawanyika makundi mawili ambayo ni TB ya ndani ya mapafu na nje ya mapafu huku akitaja dalili kuu kuwa ni pamoja na kikohozi, kupungua uzito, homa ya mara kwa mara, kutokwa jasho kwa wingi hasa mgonjwa anapokuwa amelala na kukohoa damu.

“Ndiyo maana watu wanaohudumia ama kuishi na wagonjwa wa TB wako hatarini zaidi kuugua ugonjwa huo, tunashauriwa kujikinga wakati wote kwa kutumia ‘maski’ tunapokuwa kwenye mikusanyiko. Pia, kama una historia ya kuhudumia mgonjwa basi ni vyema ukapime pia,” amesema Dk Mgallah.

Daktari huyo amesema watu wenye dalili hizo wanatakiwa kufika hospitalini kufanyiwa uchunguzi na kuanza matibabu huku akisisitiza kwamba matibabu yake yanatolewa bila malipo katika vituo vyote vya afya nchini.

Hali ya TB Ilemela

Dk Mgallah amesema kuna ongezeko la wagonjwa wa TB walioibuliwa na kutibiwa wilayani humo kutoka wastani wa wagonjwa 575 mwaka 2022 hadi 780 mwaka 2023.

Amesema ongezeko hilo linachangiwa na kuongezeka kwa uelewa katika jamii kuhusu TB huku akidokeza hamasa katika vyombo vya habari na mashujaa wanachangia kuongeza namba ya wagonjwa wanaofika na kufanyiwa uchunguzi wa TB hospitalini kisha kuanza matibabu.

“Hawa mashirika, taasisi na mashujaa wamekuwa na mchango mkubwa sana kutusaidia kuibua wagonjwa wa TB. Tunaendelea kushirikiana nao ili kufikia lengo la kutokomeza kabisa ugonjwa wa TB katika nchi yetu,” amesema daktari huyo.

Chanzo: mwanachidigital