Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shughuli anazoweza kufanya mtoto wakati wa likizo

33351 Pic+likizo Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Likizo imeanza. Hiki ni kipindi chenye msisimko wa aina yake kwa watoto. Msisimko huo, pamoja na mambo mengine, unatokana na ukweli kuwa sasa mtoto anaweza kufanya kitu kingine baada ya miezi mingi ya pilika za shule.

Pamoja na uzuri wake, shule huchosha akili na mwili. Shule zetu, kwa kulitambua hili, zimempa mtoto fursa ya kupumzika kusudi akusanye nguvu kwa ajili ya kuanza muhula ujao akiwa na nguvu na ari.

Katika macho ya mtoto hiki ni kipindi cha kufurahia uhuru. Tofauti na shuleni ambako maisha huongozwa na sheria ngumu, nyumbani kunaonekana kuwa sehemu yenye uhuru wa mtoto kufurahia maisha yake bila kufuatiliwa kwa karibu na walimu.

Wapo watoto wanaoamini, mathalani, wakiwa nyumbani wataamka muda wanaoutaka wao, watatazama televisheni, watatumia simu na mitandao ya kijamii kwa uhuru. Likizo kwao ni kipindi cha takribani mwezi mmoja wa kufanya yale waliyoshindwa kuyafanya wakiwa shuleni.

Hapa ndiko uliko umuhimu wa mzazi kuwa makini na kutoa mwongozo mapema. Nafahamu familia zetu zinatofautiana katika malezi. Kuna wazazi wanaopenda kuona watoto wakifanya mambo yao kwa uhuru. Lakini pia wapo wanaotengeneza sheria ngumu kidogo kutawala maisha ya watoto wao.

Pasipokuingilia mitazamo na misimamo ya familia, tunaweza kukubaliana umuhimu wa kuwa na utaratibu unaoongoza shughuli za mtoto awapo nyumbani. Ni vizuri, kwa mfano, ifahamike, muda wa kuamka ni upi, muda wa kushiriki kazi za mikono ni upi, muda wa kwenda ibadani ni upi na hata muda wa kurudi nyumbani kutoka matembezeni ni upi. Utaratibu kama huu unajenga nidhamu iliyoanza kujengwa kuanzia shuleni.

Pamoja na ukweli kwamba watoto wanatamani kuwa huru zaidi kuliko walipokuwa shule, ipo haja ya kudhibiti kidogo uhuru huo kulingana na umri wa mtoto. Ikiwa nafasi na umri vinaruhusu, si vibaya mtoto kutumia simu yake binafsi. Hata hivyo, ni vyema kuwa mwangalifu ili mtoto aelewe mipaka ya matumizi hayo. Uhuru holela unaweza kuzaa yasiyotarajiwa.

Sambamba na kudhibiti kidogo uhuru huo, ni muhimu kumpunguzia mtoto shinikizo la masomo katika kipindi hiki cha likizo. Nafahamu wazazi tunayo matarajio makubwa kwa watoto wetu. Inapotokea, mathalani mtoto hafanyi vizuri shuleni, saa nyingine tunalazimika kuwatafutia masomo ya ziada ili kuwasaidia kutumia kipindi hiki kujinoa zaidi.

Pamoja na nia nzuri ya kufanya hivyo, ni muhimu kuelewa kuwa akili ya mtoto huchoka. Mapumziko ni pamoja na kufanya kitu kingine cha tofauti kipindi hiki cha likizo. Badala ya kumpeleka mtoto wa darasa la kwanza ‘tuisheni’, kwa mfano, kwa nini tusitafute shughuli nyingine changamshi zisizochosha akili yake? Fikiria michezo, matamasha ya watoto, shughuli za mikono zinazomfunza stadi mbali mbali za maisha na kushiriki shughuli nyingine ambazo si tu hazimchoshi mtoto kiakili lakini pia zinamfundisha elimu muhimu nje ya madarasa. Unaonaje?



Chanzo: mwananchi.co.tz