Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheria yaongeza umri wa mtoto bima ya afya hadi miaka 21

Umri Pc Data Bima ya Afya

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: Mwananchi

Bunge limepitisha Muswada wa sheria mbalimbali, ikiwemo ya Mfuko wa Bima ya Afya, inayoongeza umri wa watoto wategemezi kwenye bima ya afya kutoka miaka 18 hadi 21.

Mbali na hilo, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) sasa inaruhusiwa kutengeneza dawa.

Sheria hizo zimo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2021 ambao ulipitishwa ijumaa Septemba 3,jioni na Bunge na sasa unasubiri kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan uwe sheria kamili.

Awali, Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, mtoto alitambulika kwa umri usiozidi miaka 18, hivyo watoto waliokuwa wakitumia kadi za bima za wazazi wao walipozidi umri huo hawakuruhusiwa kuendelea kutumia kadi hizo.

Kwa marekebisho hayo, watoto wataendelea kutumia kadi za bima za afya zinazotokana na wazazi wao hadi watakapotimiza miaka 21.

Hata hivyo, matarajio ya wabunge wengi ilikuwa uwasilishwe muswada unaoruhusu bima kwa wote.

Akichangia mjadala wa mabadiliko hayo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Salome Makamba alilalamika kwamba muswada huo umewasilishwa vipandevipande, tofauti na ilivyoahidiwa na Serikali katika Bunge la Bajeti.

Makamba amesema Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama aliahidi Serikali ingeleta muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote.

Amesema tofauti na ilivyoahidiwa vimeletwa vipandevipande na hakuna hata kipengele cha bima hiyo kwenda hadi kwa wazazi.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema katika suala la wazazi kuwemo kwenye bima ya afya, kuna baadhi ya watumishi bima zao zinahudumia hadi wazazi.

Pia, Bunge limeifanyia mabadiliko Sheria ya Idara ya Bohari ya Dawa kwa kuiongezea majukumu MSD ya kuanza kutengeneza baadhi ya dawa.

Kwa mujibu wa sheria, MSD ilikuwa na jukumu la kusambaza tu dawa, lakini sasa itaweza kutengeneza baadhi ya dawa, ambazo hata hivyo hazikutajwa.

Pia, Bunge limefanyia marekebisho Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ambapo imeongezwa fursa kwa wenye vipaji kupata elimu hata kama hawajaenda shule.

Mbunge wa viti maalumu, Agnesta Lambart amesema MSD haikupaswa kuongezewa jukumu kwa kuwa ilishindwa kusambaza dawa.

Amesema MSD ilionyesha udhaifu katika usambazaji wa dawa, hivyo haoni sababu ya kuongezewa kazi nyingine ya kuzalisha dawa.

Mjadala mwingine mkubwa ulikuwa kuu ya muswada wa Veta uliohitimishwa kwa Mhagama ambaye pia ni mnadhimu wa Serikali bungeni kusema Serikali imepokea maoni ya wabunge na kwamba kwa kuwa sasa kuna mjadala wa elimu itakapofika bungeni wataangalia namna gani ya sera na sheria kulingana na mazingira yaliyopo sasa.

Chanzo: Mwananchi