Serikali inatarajia kutunga sheria itakayoruhusu wananchi kuchangiana viungo vya ndani ya mwili ikiwamo figo.
Vilevile, imeitaka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa waadilifu kwenye sampuli zinazohusu ubakaji na vinasaba vya uhalali wa mtoto.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyasema hayo jana jijini Dodoma kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la mamlaka hiyo.
Alisema Wizara hiyo inaona kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususani kwa vijana na watoto.
"Kuna ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa ya kisukari, ya moyo, shinikizo la damu na saratani na magonjwa ya afya ya akili, bahati mbaya magonjwa haya ukiweza kuzingatia maelekezo ya wataalamu unaweza kuyadhibiti na usipofuata utaweza kuishi nayo na ni gharama kubwa.
"Kwa mfano, ukisafisha figo ni kati ya Sh. 180,000 hadi 200,000 kwa siku na bahati mabaya madaktari wetu wakiona una bima ya afya wanaweza kukuambia hata mara tano kwa wiki.
"Au upate mtu wa kukuchangia figo na Tanzania hatuna sheria ya kuchangia viungo, tunataka kuitunga," alisema.
Kuhusu uadilifu, Waziri Ummy alisema watumishi wa mamlaka hiyo wanapaswa kuwa waadilifu na kutenda haki wanaposhughulikia sampuli za jinai na ubakaji na za kupata uhalali wa mtoto.
"Ninaomba tuwe waadilifu, kwa mama haina shida maana mtoto anakuwa tumboni kwake lakini kwa baba ni shida na watoto wanateseka huku mtaani, wanaume wengi wanatelekeza watoto," alisema.
Aliishauri mamlaka hiyo kutoa elimu kwa jamii namna njema ya kutumia huduma za mamlaka hiyo katika kutafuta haki kwenye masuala ya familia na uzazi.
Kadhalika, Ummy alitaka mamlaka hiyo kuangalia namna ya kusaidia kupima uchafuzi wa mazingira wa kelele na mitetemo ambayo imekuwa tatizo kubwa kwa sasa.
Awali Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko alisema ujenzi wa jengo hilo ni mwitikio wa serikali wa kuhamia Dodoma na kupanua wigo wa huduma za mamlaka na limejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 8.1.
Alisema jengo litakuwa na maabara nane za vinasaba vya binadamu, maabara ya vinasaba vya wanyama na wanayamapori, sumu, microbiology na bidhaa za mazao na mazingira.