Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh6 bilioni zajenga vyumba vya upasuaji Mwanza

54639 Pic+mwanza

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katika kukabiliana na vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua, Serikali imesema imepeleka jumla ya Sh6 bilioni kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa vituo 14 vya afya jijini Mwanza.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Josephat Kandege ameliambia Bunge mjini Dodoma leo alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maria Kangoye aliyetaka kujua Serikali inafanya nini kukabiliana na changamoto ya baadhi ya vituo kukosa vyumba vya upasuaji.

"Kwa mwaka wa fedha 2017/18 na 2018/19 Serikali imepeleka kiasi cha Sh6 bilioni jijini Mwanza ili kukabiliana na vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua kwa kutofanyiwa upasuaji. Vituo 11 vilivyokuwa havifanyi upasuaji vitaanza kutoa huduma hiyo," amesema Kandege.

Naibu waziri huyo amesema kuwa Mkoa wa Mwanza una hospitali sita, vituo 35 vya afya na zahanati 231, lakini huduma ya upasuaji ilikuwa inapatikana kwenye hospitali pamoja na vituo 10 vya afya.

Mwaka 2018/19, Kandege amesema, Serikali imepeleka Sh3 bilioni mkoani humo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya ya Ilemela na Buchosa ambazo zikikamilika zitafanya upasuaji wa dharura kwa wajawazito, hivyo kutanua wigo na kuboresha huduma.

Licha ya vyumba, awali Maria aliitaka Serikali kupeleka wataalamu wa kutosha kwenye vituo vinavyofanya upasuaji ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Related Content



Chanzo: mwananchi.co.tz