Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh125 milioni zamwagwa kuokoa maisha ya watoto wenye saratani Dar

11120 Sh+125+pic.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Mohammed Dewji imetoa msaada wa Sh125 milioni kwa Kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ili kugharamia matibabu ya watoto wanaoumwa saratani.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo, meneja mradi wa taasisi hiyo, Rachel Chengula alisema msaada huo ni mwendelezo wa misaada ambayo wamekuwa wakiitoa kwa kituo hicho.

Alisema kuwa wanatambua hali ngumu wanayopitia watoto hao, na kwamba misaada hiyo itasaidia kuboresha huduma na kuwawezesha waliopo mikoani kusafirishwa ili kuweza kupata matibabu katika hospitali hiyo.

“Kama upo hai na mwanao anapumua mshukuru Mungu kwa kuwa ana makusudi na wewe na ana makusudi na mtoto wako. Usikatishwe tamaa na magonjwa, tunaamini kwamba watoto hawa watapona na kurudi nyumbani, watasoma na watalitumikia Taifa letu,” alisema Rachel.

“Mohammed Dewji amekuwa akifanya kazi na Tumaini la Maisha tangu mwaka 2012 ili kusaidia watoto kupatiwa matibabu. Kupitia taasisi yake tutaendelea kushirikiana ili kusaidia watoto wetu wapate matibabu.”

Meneja wa wafadhili wa Kituo cha Tumaini la Maisha, Alex Kaijage aliishukuru taasisi hiyo kwa msaada waliowapa na kuwaomba waendelee kuwasaidia watoto wenye saratani.

“Fedha hizi tunazitumia si kwa usafiri tu, hata dawa pia, kwa sababu yenu watoto wanapata matibabu na kupona. Tunawashukuru kwa kweli,” alisema.

Mmoja wa wazazi mwenye mtoto anayepatiwa matibabu ya saratani, Hams Samweli aliwataka watu wenye uwezo kifedha kujitokeza kutoa misaada ili kuwasaidia watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa huo.

“Kufanya hivyo ni kuwasaidia watoto ambao wazazi wao hawana uwezo,” alisema Samweli.

Chanzo: mwananchi.co.tz