Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh10bilioni zaokolewa kwa wagonjwa kutotibiwa nje

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa (Moi) imebainisha kuokoa Sh10 bilioni baada ya kufanya upasuaji kwa wagonjwa 1,500 waliopaswa kupelekwa nje ya Tanzania mwaka 2018 kwa ajili ya matibabu.

Idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mwaka 2018 imeongezeka hadi kufikia 7,000 ikilinganishwa na wagonjwa 5,000 waliofanyiwa upasuaji miaka miwili iliyopita.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 31, 2018 na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Moi, Dk Samwel Swai wakati akitoa tathmini ya ufanyaji kazi kwa taasisi hiyo kwa 2018.

Dk Swai amesema miongoni mwa wagonjwa waliopaswa kufuata matibabu nje ya nchi ni pamoja na wale waliohitaji kufanyiwa upandikizaji wa nyonga bandia.

Wengine ni wa upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, upasuaji mkubwa wa mgongo na ubongo, upasuaji wa kurekebisha mfupa wa kiuno.

Magonjwa mengine ni upasuaji wa mifupa kwa watu wazima na watoto, upasuaji wa kuzibua njia za maji kichwani kwa kupitia matundu kwa watoto (ETV).

"Hiyo inatokana na jitihada zilizofanyika katika kuboresha huduma za afya nchini hususani huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, Mgongo, Mishipa ya Fahamu na magonjwa ya ajali," amesema Dk Swai.

"Kutokana na wagonjwa wengi kufanyiwa upasuaji nchini katika mwaka 2018, idadi ya waliopelekwa nje kufanyiwa matibabu hawazidi 50 na tuna imani mwaka ujao itapungua zaidi,’’ ameongeza Dk Swai.

Amesema mwaka 2019 pia wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma kwa wagonjwa kupitia mpango mkakati ujulikanao kama Tiba kwa wakati ili kuhakikisha kila mgonjwa anayefika Moi anapata huduma bora na kwa wakati.



Chanzo: mwananchi.co.tz