Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yazindua utafiti viashiria vya UKIMWI

HIVandAIDSbasics Serikali yazindua utafiti viashiria vya UKIMWI

Fri, 30 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania imezindua utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania kwa mwaka 2022/23.

Utafiti huo utakaoanza Oktoba 2022, utasimamiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OSGS), Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Tume ya Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (Zac).

Pamoja na Wizara ya Afya kwa usaidizi wa kitaalamu kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magojwa cha Marekani (CDC) na Chuo Kikuu cha Colombia  Marekani (ICAP) kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Akizindua utafiti huo, jana Alhamisi, Septemba 29, 2022 jijini Mwanza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene aliyemuwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamilia kudhibiti maambukizi ya VVU kwa kuongeza uelewa kwa wananchi, kujua hali zao za maambukizi ya VVU, kujiunga na huduma za matibabu ya VVU na kuongeza ujuzi wa kukabiliana na virusi vya Ukimwi nchini.

"Tanzania inaendelea kukusanya takwimu bora ambazo zitatupa uelewa mzuri wa hali ya maambukizi katika nchi yetu," amesema

Amewataka watafiti watakaokwenda kukusanya taarifa, wakusanye taarifa bora na sahihi zitakazoleta tija,

Waziri huyo ameitaka wizara ya afya, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na wananchi kutoa ushirikino wakati wa utafiti ili kuufanikisha kwa maslahi ya Taifa.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk John Jingu amesema utafiti huo ni wa tano tangu waanze kufanya utafiti ambapo tafiti zingine zilifanyika 2003/4, 28/9, 2012/13 na 2016/17.

“Lengo ni kupata takwimu ambazo zitatuongoza katika mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi,” amesema Dk Jingu

Mkurugenzi Mtendaji wa ICAP nchini, Haruka Maruyama amesema utafiti huo utahusisha kaya 20,000 zilizochaguliwa kwa sampuli wakilishi ambapo inakadiriwa watu 40,000 wenye umri kati ya miaka 15 na kuendelea watashiriki katika utafiti huo.

Amesema lengo la utafiti huo ni kutathimini ushamiri na maambukizi mapya ya VVU na matokeo ya huduma za VVU katika jamii pamoja na kuangalia maendeleo ya malengo ya Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti Ukimwi (UNAIDS) 95-95-95.

Barozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Donald  Wright amesema utafiti huo utafanyika kwa kutumia dodoso la kukusanya taarifa na upimaji wa VVU, homa ya ini B na homa ya ini C kwa hiari na kudai kuwa watakaobainika na VVU wataunganishwa na huduma za tiba na matunzo mapema.

“Watakaoshiriki watasaidia Serikali na wadau wengine kuboresha huduma za Afya, sera na programu za kudhibiti maambukizi ya VVU nchini Tanzania,”amesema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Leonard Maboko amesema tafiti hizo ambazo ufanyika kati ya kila baada ya miaka minne na mitano ni muhimu kwakuwa ndiyo tafiti kuu wanazozitumia kueleza hali ya VVU na Ukimwi.

Mtendaji Mkuu wa Nacopha, Deogratius Rutatwa ameomba watu wanaoishi na VVU/ Ukimwi kupewa nafasi ya kushiriki katika hatua zote za utafiti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live