Serikali imesema itahakikisha dawa na vifaa tiba vya magonjwa yasiyoambukiza zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifello Sichalwe, wakati wa kufunga mafunzo ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa watoa huduma za afya kutoka mikoa nane Tanzania Bara yaliyofanyika jijini Dodoma.
Dk. Sichalwe amesema kuwa serikali, kupitia Wizara ya Afya imechua hatua ikiwemo ya utekelezaji wa mkakati jumuishi wa III wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza 2021/2026.
“Mkatati huu unahuisha kuhakikisha watoa huduma wanapewa mafunzo, ili waweze kutoa huduma bora kote nchini katika ngazi zote za uhitaji huduma za afya.”
Pia Mganga Mkuu wa Serikali aliwataka watoa huduma hao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi, ili wachukue tahadhari na kuepuka magonjwa hayo.
Alitoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kubweteka na hivyo kuchuchua tahadhari ya kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, moyo na mengine na kuhimiza kufanya mazoezi, kula mlo kamili na kuacha kutumia vileo kupita kiasi pamoja na kuacha matumizi ya tumbaku.