Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawataka wazalishaji wa dawa duniani kuwekeza Tanzania

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imetoa fursa kwa wazalishaji wa dawa duniani kuja kuwekeza viwanda vyao hapa nchini huku ikiwahakikishia soko kwani mahitaji ni makubwa.

Kauli hiyo inakuja wakati kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imeongeza bajeti ya dawa muhimu mpaka kufikia Sh296 bilioni.

Akizungumza mwanzoni mwa wiki kwenye mkutano kati ya Bohari ya Dawa (MSD), wazalishaji na wasambazaji 160 wa dawa kutoka nchi mbalimbali duniani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema mahitaji ya dawa nchini yanatengeneza fursa ya kibiashara kwa wawekezaji hao.

Alisema uwepo wa viwanda hivyo utarahisisha upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu.

“Njooni muanzishe viwanda hapa nchini, utashi wa kisiasa upo kwa sababu Serikali inahamasisha uanzishwaji wa viwanda. Tumieni fursa hiyo, Serikali ina utashi wa kisiasa kwenye viwanda,” alisema katibu mkuu huyo.

Kiongozi huyo aliwataka wazalishaji wa dawa kugeuza changamoto kuwa fursa na wahakikishe wanafanya biashara safi kwa kulipa kodi na kuzingatia taratibu nyingine za nchi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Wakati wa kufungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya alisema MSD imejiimarisha na kujijengea uwezo wa kuwahudumia wateja wake, hivyo inapaswa kuwa na uhakika na upatikanaji wa dawa zenye viwango na ubora unaokubalika.

“Lengo letu ni kuitikia wito wa Rais John Magufuli aliyetutaka kununua dawa kutoka kwa wazalishaji wenyewe badala ya kuwatumia madalali, tulishaanza kufanya hivyo na sasa tunahitaji wawekeze viwanda ndani ya nchi,” alisema Dk Ulisubisya.

 

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema mkutano huo ni hatua muhimu ya kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa pande zote mbili wakati wa manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuboresha na kurahisisha mazingira ya kibiashara.

Jumla ya wazalishaji 130 kutoka zaidi ya nchi 25 wameshiriki mkutano huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz