Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa tamko uboreshaji maadili vyuo vya afya

3fbf4a1348cd68d78d0215b1cb5ef196 Serikali yatoa tamko uboreshaji maadili vyuo vya afya

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MGANGA MKUU wa Serikali Profesa, Abel Makubi ameagiza uongozi wa chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na vingine nchini, kuboresha maadili ikiwamo lugha na mavazi kwa wanafunzi wanaopita katika vyuo vya afya.

Profesa Makubi alisema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Muhas alipofanya ziara ya kujionea shughuli zinazoendelea katika chuo hicho ikiwamo utafiti wa miti dawa itayosaidia kupambana dhidi ya magonjwa yakuambukiza na yasiyoambukiza nchini.

"Imefika mahali ambapo maadili ya baadhi ya wanafunzi wetu ambao wanamaliza vyuo vikuu halafu wanakuja kufanya kazi kwenye hospitali yamekuwa changamoto za kitabia, kukosa heshima,uvaaji na kukosa nidhamu ya kazi, na ndiyo maana nimeomba wasajili wawe hapa ili kuonesha msisitizo suala la maadili, tusiishie kwa wanafunzi ambao wamemaliza" alisema.

Alisema, ifike muda utengenezwe mwongozo wa jinsi ya kuvaa na matumizi ya lugha, nidhamu ya kuwajibika na tabia jambo litakalosaidia kuboresha maadili mbele ya kila mtu bila kuangalia rika au jinsia katika maeneo ya kutolea huduma za afya.

"Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi sana kuhusu tatizo la maadili linalofanywa na baadhi ya watumishi wetu wachache jambo ambalo ni kinyume na taaluma zetu katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi," alisema.

Profesa Makubi aliwataka wataalamu hususan walimu wa chuo hicho kutumia taaluma zao kwa kujitokeza katika jamii kutoa elimu kuhusu njia za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kuijenga jamii yenye afya bora.

Aliviagiza vyuo vikuu vya afya kuangalia namna ya kutilia mkazo somo la uongozi, uwajibikaji na utawala kwa watumishi wa sekta afya ambao baadaye ndiyo wanaweza kuwa waganga wakuu wa wilaya, mikoa na wafawidhi wa hospitali.

"Suala la utawala wa afya kwa maana ya uongozi na uwajibikaji ni kipaumbele cha kisera kwa mwaka huu baada ya kugundua baadhi ya taasisi na hospitali zinakwama kwa sababu ya uongozi usiojitambua, usiowajibika , usio na matokeo, uzalendo na kukosa umoja miongoni mwa watumishi," alisema .

Alisema Serikali itaendelea kutoa udhamini kwa wataalamu hao kuboresha huduma kwa wananchi kwa kutoa huduma za kibingwa ndani ya nchi, na kupunguza gharama za matibabu ambazo zingetumika kwa matibabu ya nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz