Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa bil 3/- vituo vya afya Kilwa

0a6c216e04d8481dcb2cdb9b445be1cc Serikali yatoa bil 3/- vituo vya afya Kilwa

Sat, 24 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 3.02 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Ilulu Njianne katika kata ya Tingi na Kivinje kwenye mikutano iliyofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi.

Alisema vituo vya afya vilivyojengwa kwa fedha hiyo ni Masoko, Pande, Tingi na Somanga ambavyo vyote vinatoa huduma na Kituo cha Afya cha Nanjilinji ambacho ujenzi wake uko kwenye hatua za mwisho kukamilika.

Akielezea kuhusu uboreshaji wa afya, Majaliwa alisema Sh milioni 403 zimetolewa na serikali kuboresha hospitali ya wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa duka la dawa na jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya Kinyonga. Alisema ujenzi wake upo katika hatua za ukamilishaji.

Kuhusu uboreshaji wa zahanati, alisema Sh milioni 164.7 zimetolewa kwa uboreshaji wa zahanati za Rushungi na Songomnara. Kwenye ununuzi wa dawa, alisema Sh bilioni 1.43 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo wastani wa fedha za ununuzi wa dawa kwa mwezi ni Sh milioni 23.9.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Lindi kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge wa majimbo ya Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane na Ally Kasinge wa Kilwa Kusini, pamoja na wagombea udiwani wa kata za majimbo hayo wa CCM.

Akielezea kuhusu sekta ya maji, Majaliwa alisema Sh bilioni 7.5 zimetolewa kwa miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi wa utafiti wa maji na uchimbaji visima katika vijiji 19, Mradi wa kuboresha huduma ya maji Kilwa Masoko, ujenzi wa mabomba Somanga na Pande na ujenzi wa mabomba Njia Nne.

"Fedha hizo zimetumika kufanya ukarabati wa mradi wa maji Kipatimu, ukarabati wa mradi wa maji Mandawa, mradi wa maji ya bomba na uvunaji wa maji ya mvua Mingumbi-Miteja, ukarabati wa mradi wa maji Kijiji cha Kipindimbi, ukarabati wa pampu za mkono 25 katika vijiji 12 vya Kilwa pamoja na mradi wa maji ya bomba Shule ya Sekondari Kinjumbi," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz