Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatanua wigo kukabili Corona

9713fbabf27ad09d93b942bbaa845516.jpeg Serikali yatanua wigo kukabili Corona

Wed, 22 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema ina mpango wa kujenga mitambo 55 ya hewa ya oksijeni kwa ajili ya kusaidia mapambano ya ugonjwa wa Covid-19 ambapo saba tayari imeshajengwa na inatumika na 12 iko katika hatua ya kujengwa.

Pia imeongeza uwezo wa kupima Covid-19 kutoka maabara moja na sasa ina vituo sita katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza.

Sambamba na hayo, imebainisha kuwa ina jumla ya dozi za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 milioni 4.42 na inatarajia kuchanja takribani asilimia 60 ya Watanzania ambayo ni sawa na watu milioni 35.

Hayo yalielezwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waratibu wa afya wakiongozwa na waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu uhamasishaji wa utoaji chanjo.

Leo kampeni kabambe awamu ya pili ya uhamasishaji chanjo dhidi ya Covid-19 inazinduliwa jijini Arusha ikiwa na lengo hilo la kuchanja asilimia 60 ya Watanzania.

Katika semina hiyo ilielezwa kuwa hadi Kufikia Desemba 18 mwaka huu watu 28,214 walithibitika kuwa na maambukizi ya Covid-19 na 739 wamepoteza maisha. Semina hiyo inafanyika ikiwa ni maandalizi ya kampeni ya uhamasishaji

juu ya chanjo itakayofanyika nchi nzima kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanajitokeza kwa wingi kuchanja ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo ya pili.

Alisema kampeni hiyo ya pili inazinduliwa kutokana na ukweli kuwa kampeni ya kwanza haikufanya vizuri sana lakini pia kwa sasa kuna tishio zaidi la maambukizi ya corona.

“Katika kampeni ya kwanza tulianza vizuri sana lakini baadaye hali ilisuasua ndipo tukaanza kampeni ya kuhakikisha Watanzania wanajikinga vyema na Covid-19 kwa chanjo na afua nyingine kama kuvaa barakoa nakadhalika,” alisema Dk Sichalwe.

Alisema pamoja na suala hilo la chanjo serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na janga hilo kama vile kushirikisha jamii katika kupambana na Covid-19 kwa kutoa elimu na kuimarisha ufuatiliaji wa hali ya ugonjwa kwenye viwanja vya ndege, majini na mipakani.

Hatua nyingine alizotaja ni kutoa tiba kwa waathirika, mafunzo kwa watumishi na uimarishaji wa upatikanaji wa hewa ya oksijeni ambapo kuna mpango wa kusimika mitambo 55 ya hewa ya oksijeni nchi nzima.

Alisema pia serikali imechukua hatua ya kuhakikisha dawa zinapatikana na kuongeza wigo wa upimaji wa corona na utoaji wa chanjo.

Kwa upande wake, Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk Florian Tiruga alisema ugonjwa huo ulipoingia nchini asilimia 80 ya Watanzania waliugua na kutibiwa, asilimia 15 walilazwa na asilimia tano walilazwa katika wodi za magonjwa mahututi (ICU).

“Chanjo hupunguza makali ya ugonjwa, inaondoa mgonjwa kulazwa ICU lakini pia tukumbuke inakwenda sambamba na afua nyingine kama kuvaa barakoa, kuepuka msongamano na kunawa mikono na maji tiririka,” alisema.

Alisema katika kampeni ya kwanza mikoa takribani 10 haikufanya vizuri kama vile Tanga, Manyara, Singida, Tabora, Lindi na Katavi hivyo kampeni ya pili itaelekeza nguvu katika mikoa hiyo ili kupata mwitikio chanya.

Hata hivyo, alisema hadi kufikia mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, jumla ya Watanzania 973,728 sawa na asilimia 92 walichanja chanjo ya Janssen. Alisema kwa sasa zimeongezeka chanjo aina mbili zaidi ikiwemo Janssen, Sinopharm na Pfizer.

Alisema kati ya asilimia 60 ya Watanzania wanaotarajiwa kuchanja katika kampeni ya pili tayari asilimia 2.24 wameshachanja.

Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Antony Keya aliwataka wataalamu watakaokwenda kuhamasisha jamii kuhusu chanjo kutumia utaalamu wao na kuwaelimisha wananchi kwa lugha laini ili waelewe.

Semina hiyo imeandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kinga kitengo cha elimu ya afya kwa umma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live