Dodoma. Serikali imetakiwa kuweka utaratibu maalum wa
kuhamasisha watu kujitolea kuchangia figo kwa kuwa mchakato wa kupatakiungo hicho ni mgumu kwa sababu haziuzwi.
Wito huo umetolewa leo Agosti 30 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Egid Mubofu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na huduma mbalimbali za kibingwa zinazotolewa na Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo chuoni hapo.
Amesema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma ya kupandikiza figo tangu Machi mwaka huu lakini mchakato wa kuzipata
figo hizo umekuwa mgumu kwa sababu haziuzwi bali zinategemea mtu
kujitolea kwa kupenda.
"Hakuna fedha yoyote inayoweza kununua kiungo cha binadamu hivyo naiomba Serikali iweke utaratibu maalum wa watu kuchangia viungo vyao kama figo kwa ajili ya kuwapa watu wengine wenye uhitaji wa viungo hivyo kwa sababu haviuzwi," amesema Profesa Mubofu.
Amesema upatikanaji figo kwa sasa unategemea ndugu kujitolea kwa
hiari hivyo kufanya nchi kuwa na wagonjwa wengi wa figo lakini
wanaojitolea ni wachache na kwamba kukiwa na utaratibu maalum wa
kuchangia viungo hivyo kutapunguza vifo vitokanavyo na maradhi ya
figo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk
Alphonce Chandika amesema mpaka sasa hospitali hiyo imeshapandikiza figo wagonjwa wanne ambao wanaendelea vizuri na kwa sasa ina mpango wa kuwasomesha madaktari bingwa wengine kwa ajili ya kufanya upasuaji wa magonjwa ya moyo.
Amesema lengo ni kuwawezesha Watanzania wanaohitaji matibabu ya
kibingwa kuyapata hapa nchini kwa gharama nafuu tofauti na kupelekwa
nje ya nchi.
Amesema kuwa matibabu ya kupandikiza figo ndani ya nchi ni gharama nafuu ukilinganisha na ya nje ya nchi kwa kuwa huduma hii nchini ni Sh22 milioni na wakati kwa matibabu hayo hayo nje ya nchi ni zaidi ya Sh80 milioni.
Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk, Kessi Shija amesema kuwa serikali ikiweka utaratibu mzuri wa watu kuchangia viungo vya binadamu viungo hivyo pia vitawezekana kupatikana hadi kutoka kwa marehemu.
“Hili zoezi la kupandikiza figo linafanyika kwa mujibu wa sheria kwa kuwa linahusisha kumfanyia upasuaji mtu ambaye si mgonjwa sasa kwa
sheria hiyo hiyo kama serikali itaridhia tutaweza kuvuna figo kwa
marehemu kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kuwapandikizia
wahitaji,” alisema Dk, Shija.