Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yataka utayari watumishi wa afya

D4073a294302aac549af31c094d10f0f Serikali yataka utayari watumishi wa afya

Tue, 22 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imewataka watumishi wa afya kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani zimekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 kwa kuwa raia wa nchi hizo wana mwingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara na Tanzania.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichalwe alisema hayo jana Dar es Salaam baada ya kufanya ziara fupi katika Hospitali ya Amana kukagua utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Covid-19.

Alikagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi.

Katika ziara hiyo, aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi zake kuzuia ueneaji wa maambukizi.

Pongezi hizo zilitokana na watumishi wote kukutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji zikiwapo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini.

“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi,” alisema.

Dk Sichalwe aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unakinga si tu na ugonjwa wa Covid-19, bali pia magonjwa mengine yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.

Akiwa hospitalini hapo, Sichalwe alitembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya oksijeni hospitalini hapo na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu kwa kuwekeza zaidi ya Sh milioni 600 kuhakikisha wanaokoa maisha ya Watanzania wanaohitaji huduma hiyo.

Mtambo huo wenye matoleo zaidi ya 89, una uwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksijeni kwa saa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume, alisema juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanadhibiti ipasavyo wimbi la tatu la Covid-19.

Chanzo: www.habarileo.co.tz