Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yataka Watanzania kuchangamkia bima ya afya

2c6d50a4de582f9b97e5185211232567.png Serikali yataka Watanzania kuchangamkia bima ya afya

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeanzisha kampeni kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa ili kufikia zaidi ya asilimia 20 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Ntuli Kapologwe, takribani asilimia 80 ya Watanzania hawajajiunga na huduma za bima ya afya.

Hadi sasa takriban asilimia 5 ya Watanzania ndio waliojiunga na CHF iliyoboreshwa, huku waliojiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wakiwa asilimia nane na bima binafsi asilimia 1.

Dk Kapologwe alibainisha hayo jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za serikali kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya sambamba na uimarishaji wa huduma za bima ya afya.

Alisema, lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo ili wanapougua wapate matibabu hata kama watakuwa hawana fedha mkononi.

“Tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wasiokuwa na bima wanapata shida wanapohitaji huduma za afya kwa kukosa pesa za papo kwa papo, lakini mfuko huu utawawezesha kupata matibabu katika hospitali yoyote ya serikali eneo lolote nchini,” alisema.

Alisema kampeni hiyo inatokana na serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na kuboresha miundombinu na vifaa tiba ili watu wajiunge na kuwa na uhakika wa matibabu wanapougua.

“Tunataka wananchi wengi wajiunge ili vituo vya afya viweze kujitegemea na kujiendesha vyenyewe kutokana na michango ya wananchi maana serikali pia inajazia kiasi fulani,” alisema.

Akaongeza: “Hadi sasa uchangiaji katika mfuko huu ni asilimia tano na kaya zilizojiunga ni 557,000 zenye wanufaika milioni 3.3; bado ipo haja wananchi kujiunga kwani mfuko huu ndio mkombozi wao katika masuala ya matibabu na tunataka hadi mwakani mwezi kama huu, tuwe tumefikia asilimia 20 ya uchangiaji.”

Alisema mfuko huo umefanyiwa maboresho mengi, ikiwa ni pamoja na kuongeza mafao kama ya upasuaji mdogo na mkubwa, huduma za mionzi, tiba ya mazoezi kwa waliopata kiharusi na rufani hadi hospitali kubwa nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz