Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yasaidiwa vifaa zaidi bil. 2/- kwaajili ya Corona

100861 Pic+corona+kupona Serikali yasaidiwa vifaa zaidi bil. 2/-

Sat, 20 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imepokea vifaa tiba na kinga venye thamani ya Sh. bilioni 2.9 kutoka kwa taasisi za serikali, binafsi na mashirika ya maendeleo.

Misaada hiyo ilipokelewa jijini Dar es Salaam jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Akipokea msaada huo, Prof. Makubi, alisema vifaa kinga na tiba vitasaidia utoaji bora wa huduma nchini kwa kusambazwa katika zahanati na vituo vya afya nchini.

Alisema serikali ikishirikiana na TAMISEMI imeongeza vituo vya huduma za afya nchini kutoka 7,014 hadi 8,783 na zahanati mpya 487 kwa muda wa miaka mitano.

Alisema serikali imejipanga kuimarisha vituo vya kanda na mikoa hivyo huduma bora zinahitajika ili kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya ikiwamo vifo vya mama na mtoto nchini.

Alitoa mfano wa baadhi ya misaada hiyo kama vitanda na vifaa vya chumba cha uangalizi maalumu (ICU) vya wagonjwa ambavyo vilikuwa vinahitajika kwa upande wa huduma za afya.

Ofisa Mradi wa Shirika la Plan International nchini, Peter Mwakabwale, alisema kusudio la kutoa msaada huo ni kuisaidia serikali upande wa huduma za afya hasa wafanyakazi na watoa huduma nchini ili kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mwakabwale alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni vipimia joto, miwani tiba, nguo za kazi, vitakasa mikono, barakoa, viatu na glovu vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 38.

“Kupitia mpango huu na vifaa hivi tuna uhakika changamoto za kiafya kwa watoa huduma wa afya zitatatuliwa kwa kuwa watatoa huduma kwa ubora na uhakika,” alisema.

Alisema Shirika la Plan litaendelea kusaidia serikali katika nyanja mbalimbali ikiwamo afya ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanalindwa hasa haki za watoto wa kike ambao wanaonekana kuathirika zaidi.

Baadhi ya taasisi za umma na binafsi na mashirika yaliotoa misaada mbalimbali ni pamoja na Benki ya I&M, Plan International, KOICA, Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), Kioo Limited, Stanbic Bank, Bohari ya Dawa (MSD), Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na TICTS.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live