Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapunguza rufaa matibabu nje 90%

Aaade6896037df9f84d03d2e17254f3e Serikali yapunguza rufaa matibabu nje 90%

Tue, 20 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeboresha huduma za afya zikiwemo za kibingwa na kupunguza rufaa za tiba nje ya nchi kwa asilimia 90 katika kipindi cha mwaka 2019/20.

Ofisa mwandamizi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Ahmed Makuani aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka mitano ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dodoma.

Alisema kutokana na ongezeko la huduma za kibingwa nchini mwaka jana wagonjwa wanne tu walipewa rufaa ya kwenda kupata tiba nje ya nchi.

"Hii ni kwa sababu ya uwekezaji ambao serikali imeufanya katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini," alisema Dk Makuani na kuipongeza BMH kwa kuongeza utoaji huduma za kibingwa ambazo sasa zinavutia watu kutoka nchi za nje.

Mkurugenzi Mkuu wa BMH, Dk Alphonce Chandika alisema katika kipindi cha miaka mitano hospitali hiyo imeongeza utoaji huduma za kibingwa na ubingwa wa juu zikiwemo huduma ya upandikizaji figo, usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

DK Chandika alisema wagonjwa 86 wa figo wanapatiwa huduma za kusafisha damu na jumla ya session 11,310 zikifanyika tangu kuanza huduma hiyo mwaka 2017.

"Pia Machi 2018, BMH kwa kushirikiana na washirika wa Japan, Tokushukai Medical Gropu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tulianza huduma ya upandikizaji figo, na mpaka sasa wagonjwa 13 wamenufaika na huduma hiyo na wawili kati ya hao walipandikizwa figo na wataalamu wa ndani”alisema.

Alisema pia hospitali hiyo inaendelea na kliniki ya wagonjwa waliopandikizwa figo na mpaka sasa wagonjwa 18 wanahudhuria kliniki hiyo ikiwa na wagonjwa 12 waliopandikizwa figo BMH, wawili walipandikizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wanne walipandikizwa India.

Alisema Februari mwaka huu walianzisha huduma ya kibingwa ya upasuaji wa mawe kwenye mfumo wa mkojo hususani kwenye figo kwa kutumia mawimbi na mpaka sasa wagonjwa 35 wamehudumiwa.

Kuhusu huduma ya upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, Dk Chandika alisema wagonjwa watano ambao mwili ulikuwa umekosa mawasiliano kutoka na ajali walitibiwa na wagonjwa 18 waliobainika kuwa na saratani ya ubongo walipatiwa matibabu.

Alisema Februari mwaka jana hospitali ilianzisha huduma ya ubingwa wa juu wa kutumia maabara kuchunguza na kutibu magonjwa ya moyo na kwamba, wagonjwa 223 wananufaika wakiwemo 11 waliogundulika kuwa na tatizo la kuzima mishipa ya moyo.

"Gharama ya huduma hii ni wastani wa Sh milioni 4.5 hadi milioni 6 kwa hapa nchini ikilinagnishwa na zaidi ya Sh milioni 30 hadi 40 kwa matibabu kama haya nje ya nchi, hivyo uansihwaji wa huduma hii ni dhairi unaokoa fedha za serikali."na kuongeza kuwa;

"Nimpongeza Rais John Magufuli kwa maono yake ya kuwekeza katika vituo vya kutolea huduma za avya hapa nchini, hatua ambayo inapunguza rufaa na gharama ya huduma ya afya na matibabu."

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema serikali imeboresha huduma za afya na kwamba watu sasa wanapata tiba bora za afya bila kuhitaji kwenda nje ya nchi.

"Mke wangu ni Mrusi lakini wiki iliyopita alikuwa amelazwa hospitalini hapa kwa matibabu na sasa yuko anaendela vizuri," alisema na kuongeza;

"Pia na kama si uwekezaji huu, janga la ugonjwa wa corona ambalo lililazimisha nchi zilizoendelea kufunga mipaka na usafiri wa anga, ingeweza kuongeza shida ya kiafya kwa wananchi wetu."

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga aliipongeza BMH kwa kupiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wakiwemo wanachama wa mfuko huo.

Chanzo: habarileo.co.tz