Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapiga ‘stop’ matumizi ya fomu 2C kuchukua dawa

Ummy?fit=857%2C569&ssl=1 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Sun, 3 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Serikali imepiga marufuku matumizi ya fomu za 2C zinazoruhusu kuchukua dawa kwenye maduka ya dawa kwa kutumia bima kwenye hospitali za rufaa za kanda na mikoa.

Marufuku hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akisema fomu hizo zimekuwa zikitumika kwa udanganyifu na wizi, kwani baadhi ya wamiliki wa maduka ya nje ni watendaji wa hospitali husika.

“Sababu kubwa ya kusitisha matumizi ya fomu za 2C ni kwa sababu kumekuwa na udanganyifu na wizi mkubwa, kwani watendaji wa hospitali ndio wamiliki na mgonjwa anaandikiwa dawa hakuna kumbe zipo.

“Kwa hiyo kuanzia leo (Julai mosi), tumesitisha matumizi ya fomu za 2C za Bima ya Afya ya NHIF ambazo zilikuwa zinaruhusu watu wanapokosa dawa kwenda kununua kwenye maduka mengine nje ya hospitali,” alisema.

Ummy alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mtambo wa kuzalisha gesi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa uliogharimu Sh1.1 bilioni.

Alisema hospitali zote zihakikishe kunakuwa na upatikanaji wa dawa, ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa kutafuta dawa nje ya hospitali.

“Kuhakikisha hospitali inakuwa na dawa si kazi ya mgonjwa, bali ni hospitali. Mgonjwa anatakiwa apate vipimo na dawa hospitalini na si vinginevyo,” alisema Ummy

Pia alisema ikiwa mgonjwa atafika hospitali ambayo imeingia mkataba na Bima ya NHIF, wahakikishe dawa zote zilizopo kwenye mfumo wa dawa zilizoruhusiwa zinapatikana ndani ya hospitali.

Kutokana na mfumo huo, Waziri Ummy alisema mwaka 2021 Serikali ililipa Sh25.8 bilioni kwenye maduka binafsi ya dawa yanayotumia Bima za NHIF na kueleza fedha hizo zingekwenda kwenye mapato ya hospitali zingesaidia kwenye manunuzi ya dawa, umeme, vitendanishi na maji.

Alisema mfumo huo unawanufaisha wachache, kwani maduka ya dawa 2,678 ndiyo yaliyosajiliwa na Baraza la Wafamasia, huku maduka 612 yamesajiliwa na Bima ya NHIF. Akizungumzia bima ya afya kwa wote, alisema haitamlazimisha mtu isipokuwa kutakuwa na unafuu wa kuchangia na kupata huduma kwenye hospitali kubwa kama Benjamin Mkapa na Muhimbili.

“Unalipa Sh50,000 au Sh60,000 kwa mtu na unapata huduma hospitali ya Benjamin Mkapa mpaka Muhimbili,” alisema

Awali, aliiahidi Hospitali ya Benjamin Mkapa kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Taifa kwa kuwa na sifa za kutoa huduma bora na za kibingwa kabla ya Julai 2025.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika alisema kupitia mtambo huo, Serikali itaokoa Sh 396.9 milioni endapo mitungi hiyo ingenunuliwa kutoka kwa viwanda binafsi. Alisema mtambo huo uliohusisha manunuzi ya gari la kusambazia mitungi ya gesi, mtambo, jengo umegharimu Sh 1.5 bilioni na utakuwa na uwezo wa kuzalisha mitungi ya gesi 400 kwa siku.

Chanzo: Mwananchi