Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapewa somo kusimamia usambazaji wa dawa

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Serikali kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetakiwa kuona haja ya kuingiza kanuni za sheria zinazosimamia usambazaji wa dawa (DGP) katika sheria ya kitaifa na miongozo, lengo likiwa ni  kuimarisha udhibiti wa bidhaa hizo hususani kukwepa udanganyifu kwenye soko.

Rai hiyo imetolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) leo Jumatatu Februari 25, 2019 kwenye semina ya mafunzo kwa wakaguzi wa chakula na dawa, wa mamlaka za udhibiti kutoka Tanzania na Malawi, Tanzania inawakilishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Mwakilishi wa WHO, Dk Tigest Ketsela amesema licha ya Tanzania kutambulika na shirika hilo kwa kufanya vizuri kwenye ukaguzi wa dawa na chakula, bado ipo haja ya kuingiza kanuni zinazosimamia usambaaji wa dawa kwenye sheria za kitaifa ili kudhibiti udanganyifu kwenye soko ikiwamo kuingiza bidhaa zisizo na ubora.

Amesema WHO lengo lake ni udhibiti wa dawa kwa ngazi ya Taifa na kimataifa, ikijumuisha maendeleo ya kanuni, viwango, mwongozo, msaada wa kiufundi na mafunzo ili kuwezesha nchi kutekeleza miongozo ya kimataifa kusudi kufikia malengo maalumu ya udhibiti wa chakula na dawa.

Kulingana na WHO, chini ya asilimia 30 ya mamlaka ya udhibiti wa dawa ya dunia wamefikia  uwezo wa kufanya kazi zinazohitajika ili kuhakikisha dawa, chanjo na bidhaa nyingine za afya zinafanya kazi na hazidhuru wagonjwa wanaozitumia.

Mwishoni mwa mwaka jana, (TFDA) ilitambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya WHO ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, hatua ambayo imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata mafanikio hayo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Zainab Chaula ameitaka TFDA kuhakikisha inaongeza juhudi ya utendaji kazi ili ipande kutoka ngazi ya tatu kwenda ya nne ambayo ndiyo bora zaidi.

“Nilikuwa nauliza hizi ngazi za ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa zinaishia ngapi, nikaambiwa bora zaidi ni nne, hivyo kwa nini tusipambane kuifikia hiyo ambayo ni bora zaidi, hakuna kinachoshindikana chini ya jua ni malengo na mipango tu,” alisema Dk Chaula.

“Mafunzo haya ya siku tano yatalenga namna bora ya kuhakikisha hakuna dawa isiyostahili kuingia kwenye mnyororo wa utayarishaji, usambazaji, hilo  ni jambo moja, utekelezaji ni jambo la pili.”

“Lakini muhimu zaidi elimu itakayopatikana iwafikie watumiaji wafahamu namna ambavyo wanaweza kubaini dawa, zisizo na ubora na kutoa taarifa kwa mamlaka kwa ajili ya ufuatiliaji,” amesema Dk Chaula.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TFDA,  Dk Candida Shirima amesema mafunzo hayo yatawaongezea uwezo katika udhibiti wa mfumo wa usambazaji dawa nchini, kuanzia inapozalishwa hadi kumfikia mtumiaji.

“Kama mfumo wa usambazaji hautakuwa mahiri na  kwa kuzingata mifumo sahihi ubora ufanisi na usalama wa dawa unaweza ukaathirika katika mnyororo mzima, hivyo ufuatiliaji makini unahitajika kuanzia usafirishaji, utunzaji hii itasaidia  wagonjwa kupata  dawa zenye usalama, ubora na ufanisi.” amesema Dk Shirima.



Chanzo: mwananchi.co.tz