Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaonya tiba holela ya macho

Macho Tiba Serikali yaonya tiba holela ya macho

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeonya upimaji holela wa macho sambamba na uuzaji, ugawaji wa miwani.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alitoa onyo hilo wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa macho nchini.

Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua wote watakaoendesha vitendo hivyo vya kupima macho na kugawa miwani holela.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, asilimia 20 ya Watanzania wanakabiliwa na tatizo la macho hivyo juhudi maalumu zinapaswa kuwekwa kuilinda asilimia 80 ambayo haina tatizo hilo.

"Lengo hapa ni kukabiliana na uholela wa utoaji tiba za macho, tumeona vyema kufanya hivyo ili kuondoa tatizo hilo, huko nyuma kuna mambo ambayo yalipitishwa yakitazama zaidi biashara kuliko maadili ya kitaaluma," alisema Dk Mollel.

Aidha, alisema kwa kufanya hivyo, itasaidia serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutofilisika hasa kwa kuepuka kutoa matibabu kwa watu wenye matatizo ya macho ambao pengine wasingeweza kupata tatizo hilo kama wangeepuka uholela wa ununuzi wa miwani hiyo.

Rais wa Chama cha Wataalamu wa Macho Afrika, Frank Mapuga alisema tatizo la ugonjwa wa macho linaweza kuepukika pale ambapo wataalamu waliopo katika sekta hiyo watafanya kazi zao kwa kuzingatia maadili yanayowaongoza.

Alisema Umoja wa Mataifa umeweka lengo ifikapo mwaka 2030 dunia iwe imetatua tatizo la macho. Alisema kwa nchi za Afrika suala hilo linaonekana kama si rahisi kufikiwa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Alisema katika kuhakikisha wanafikia lengo hilo, wanaweka mkazo kufikisha huduma za afya ya macho kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo, watawezesha wananchi wengi kupima na kupatiwa matibabu itakapohitajika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live