Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yanunua mashine 10 za kisasa za X-ray

20411 Ummy+pic TanzaniaWeb

Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kuboresha huduma za X- ray Tanzania Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imenunua digital X-ray mashine 10 zenye thamani ya kiasi cha Sh1.7 bilioni.

Mashine hizo zitasambazwa kuanzia leo Oktoba 2, 2018 katika Hospitali ambazo zina X-ray za zamani ambazo zimekwisha muda wake.

Akizungumza wakati wa kukagua mashine hizo leo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema katika awamu hiyo ya kwanza zitapelekwa katika hospitali nane za rufaa na mikoa.

"Mikoa iliyopewa kipaumbele ni Morogoro, Bukoba, Njombe, Katavi, Ruvuma, Simiyu, Singida pamoja na hospitali ya Rufaa ya Amana huku katika hospitali ya Chato mashine kama hiyo imeshafungwa," amesema Ummy.

Amesema mbali na kununua mashine hizo katika bajeti ya mwaka 2018/19 Serikali imepanga kununua digital X-ray mashine nyingine 24 zenye thamani ya Sh4.1 bilioni.

"Mashine hizi zina uwezo wa kupiga picha na kutoa majibu ndani ya dakika moja jambo ambalo ni haraka na kupunguza muda wa mgonjwa kukaa hospitalini," amesema Ummy.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Meshack Shimwela amesema kutolewa kwa mashine hiyo itaweza kurahisisha ufanyaji kazi katika hospitali yake kwa kiasi kikubwa.

"Hospitali yetu inahudumia watu wengi sana hivyo kupatikana kwa mashine hii itakuwa ni ahueni kwetu sisi na tutaweza kuhudumia wagonjwa wengi zaidi," amesema Shimwela.

Chanzo: mwananchi.co.tz