Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakabili corona kisayansi, kiasili *Yatumia bil 28/- kukabili ugonjwa huo

131b2760ef1f200bff9137adafb35b60 Serikali yakabili corona kisayansi, kiasili *Yatumia bil 28/- kukabili ugonjwa huo

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema inaendelea na jitihada za kukabili maambukizi mapya ya virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19 kwa kutafuta tiba mbadala, huku ikibainisha kuwa licha ya kutumia njia za asili, inaukabili ugonjwa kisayansi pia.

Imenunua mashine mbili zenye thamani ya Sh bilioni nne ambazo pamoja na kufanya vipimo vingine, zina uwezo wa kupima kiufanisi virusi vya corona na zipo katika Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza kwa ajili ya upimaji wa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Akizungumza katika kipindi cha Agenda 2021 kilichorushwa na Televisheni ya Star juzi saa 4 usiku, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel alieleza kushangazwa na watu wanaodhani hakuna Serikali inalofanya katika kukabili ugonjwa huo.

“Wapo watu wanaodhani kuwa hakuna tunalofanya yaani ni kama siye tumejikita kwenye njia za asili tu. Hapana. Serikali hii inatumia njia zote za kisayansi na asili, inatambua kuwa corona inapaswa kudhibitiwa ndiyo maana imekuwa makini zaidi kuikabili," alisema.

Alisema katika kuhakikisha azma hiyo inaendelea kuisogeza tiba asili karibu zaidi na wananchi, alitoa mfano wa huduma ya kujifukiza inayopatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema, kwa kutambua uwezo wa tiba asili katika kukabili corona, Serikali imesaidia upatikanaji wa dawa mbalimbali za tiba asili ikiwa pamoja na kuhamasisha kujifukiza, kusaidia wananchi kujipatia tiba ya haraka wakati wakiendelea na taratibu nyingine.

Vile vile alisema serikali imekuwa ikitumia wataalamu wake katika sekta ya afya, kufanya ufuatiliaji wa kina wa kisayansi wenye kulenga kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya ugonjwa huo na inaendelea kushirikiana na wadau wengine kutoka sekta binafsi.

Dk Mollel alisema serikali inaendelea kuhimiza ufanyaji wa mazoezi kukabiliana na corona na kuwataka Watanzania kuondoa hofu dhidi ya taarifa mbalimbali zinazohusu ugonjwa huo zisizolenga kuwasaidia.

Alisema wapo watu wanaosema kuwa Serikali haikusanyi takwimu za vifo vitokanavyo na corona, huku akibainisha kuwa Serikali inazikusanya isipokuwa haizitangazi.

Alisema,"tuliacha kutangaza habari za vifo vitokanavyo na corona ili kuwaondoa hofu wananchi wetu, na sasa ndiyo mataifa mengine yakiwemo makubwa, nayo yameacha kutangaza baada ya kutambua kuwa walikuwa wakiwaongezea hofu wananchi wao".

Alisema, serikali haiogopi kusema idadi ya vifo, isipokuwa inazingatia kwamba hili ni janga ambalo linahitaji umakini katika kushughulika nalo na siyo siasa, halihitaji kurushiana mpira.

Aliitaka jamii kuwapuuza watu wanaoonesha kana kwamba serikali haifanyi kitu kuhusu corona, badala yake waone namna serikali inavyotumia fedha nyingi kusaidia vita dhidi ya ugonjwa huo.

Akirejelea taarifa iliyotolewa na kiongozi mmoja wa dini ikitaja idadi ya watumishi wa kanisa waliopoteza maisha, Naibu Waziri alisema taarifa hiyo ilitoa taswira kama vile serikali haifanyi lolote katika kukabili ugonjwa huo.

Akizungumza na HabariLeo kuhusu maboresho ambayo serikali imeshayachukua katika kukabili ugonjwa huo, naibu waziri huyo alisema mashine mbili zenye thamani ya Sh bilioni nne zinaweza kupima sampuli 10,000 za corona.

Alisema zitasaidia uimarishwaji wa vipimo vya corona kwa mikoa jirani ya Mwanza na kupunguza ulazima wa vipimo kupelekwa kwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Alisema serikali inataka kuhakikisha vipimo vinafanyika kwa ufanisi na haraka zaidi, ambapo mashine hizo zitatoa majibu hata ya wageni watakaotakiwa kupima afya kabla ya kuingia nchini iwapo watalazimika kupima.

Alisema tangu kuingia kwa ugonjwa huo nchini, hadi sasa serikali imetumia Sh bilioni 28.Fedha hizo zilihusisha mambo mbalimbali ikiwamo upimaji, ununuzi wa vifaa na huduma nyingine muhimu zinazohitajika katika kukabili ugonjwa huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz