Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajipanga kujenga vituo vya ebola Kilimanjaro na Mwanza

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Serikali imejipanga kujenga vituo vya kuwahifadhi na kuwachunguza watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola katika mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi wa huduma za udhibiti wa ubora kutoka wizara ya afya Dk Mohammed Mohammed amesema licha ya kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini lakini Serikali ni lazima ichukue tahadhari.

Amesema Serikali inaanza kujenga vituo hivyo katika mikoa hiyo kwa kuwa raia wengi wa kigeni wanasafiri kupitia viwanja vya ndege katika mikoa hiyo.

 

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inajenga vituo katika maeneo mbalimbali nchini.

 

“Kwa sasa tuna Center moja ipo Temeke jijini Dar es Salaam, lakini tunatarajia kujenga vituo viingine katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro, mfano ukiangalia mkoa wa Mwanza raia wengi wa Congo wanapenda kufika mkoani hapo.”amesema na kuongeza:

“Sasa kuna ulazima wa kuweka vituo hivyo ambavyo vitatumika kuwahifadhi na kuwachunguza wale wote watakaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo,” amesema Dk Mohammed.

Amesema katika maeneo yote ya mipakani Serikali imepeleka timu ya waatalamu ambao kazi yao ni kufanya mafunzo kwa wananchi ili kuwaelimisha wananchi dalili na nini cha kufanya pindi ugonjwa huo unapotokea.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za kinga wizara ya afya Dk Leonard Subi amewatahadharisha walaji wa nyama pori hususani sokwe kuchukua tahadhari ya kutokula nyama hiyo ili kuepuka kupata ugonjwa wa Ebola.

Amesema ugonjwa wa Ebola umeibuka tena katika nchi ya  Kidomokradia ya Congo ambapo hadi sasa wagonjwa 30 wamegundulika kufariki kwa ugonjwa huo.

Amesema kutokana na ugonjwa huo kuibuka kwa mara nyingine watanzania wanatakiwa kuchukua tahadhari hasa wale wanaokula sokwe kwani mnyama huyo anatajwa kuwa na virusi vya Ebola.

Chanzo: mwananchi.co.tz