Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaipa 5 sekta binafsi ya afya

6d68d10033a0a07ed79a3936315a3893 Serikali yaipa 5 sekta binafsi ya afya

Sat, 11 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imepongeza juhudi zinazofanywa na sekta binafsi hususani uwekezaji unaofanywa katika sekta ya afya na kudai kuwa sekta hizo zimesaidia kupunguza misongamano katika hospitali za serikali.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, akizungumza katika Kongamano la Tafiti za Kisayansi, lililoangazia kuboresha mifumo ya afya na ustahimilivu yanapotokea majanga kama Covid 19 na majanga mengine.

Kongamano hilo limefanyika leo Juni 10, 2020 kwenye Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert kairuki (HKMU), Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mollel amesema uwekezaji uliofanywa na Hayati Profesa Kairuki kwenye sekta ya afya ni mkubwa na wa kuigwa kwani umesaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali za serikali.

Amesema hospitali binafsi zimekuwa na mchango mkubwa kwani zimesaidia kupunguza msongamano katika hospitali za serikali.

"Fikiria wagonjwa wanaokuja hapa Kairuki na hospitali nyingine binafsi, hizi hospitali zisingekuwepo wagonjwa wangefurika pale Muhimbili na hospitali nyingine za serikali, ni wazi serikali ingelemewa."Amesema Dk Mollel

Aidha, amesema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na familia ya Kairuki katika kuwekeza kwenye sekta ya afya kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), ambacho kimekuwa kikitoa idadi kubwa ya wataalamu wa sekta ya afya.

“Sayansi ndiyo jicho la taifa lolote duniani hivyo mchango wenu kwenye kuzalisha watalamu wa afya ni mkubwa sana na serikali inathamini kazi kubwa mnayofanya, serikali itaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono.” Amesema Dk. Mollel.

Amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye tafiti mbalimbali na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa Sh bilioni nne kwa Taasisi ya Utafiti wa Afya (NIMRI), ili waweze kutafuta chanjo za kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo Corona.

Amesema wanasayansi lazima wajipange kukabiliana na magonjwa yatokanayo na virusi kwani dalili zinaonyesha kwamba ndilo tishio kubwa duniani kwa siku zijazo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla, amesema magonjwa ya kuambukiza yamekuwa changamoto kubwa sana kwa nchi zinazoendelea kulinganisha na zile zilizoendelea.

Amesema Ukimwi bado ni changamoto kubwa ingawa kuna dawa za kufubaza virusi na mtu kuweza kuishi muda mrefu, hata hivyo mlipuko wa Covid 19 umeonyesha Dhahiri udhaifu uliopo katika sekta zote.

“Imetuonyesha udhaifu nchi zote duniani kushindwa kukabiliana na mlipuko, Desemba 2019 mlipuko ulianza China, Machi 2020 ukaingia nchini, umesambaa dunia nzima, ipo haja ya kuhakikisha mifumo ya afya inakuwa vizuri na kuweza kujitayarisha na milipuko mingine.” Amesema Profesa Mashalla.

Amesema mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 umeonyesha ni kwa namna gani taifa linapaswa kuweka mifumo imara kujiandaa kukabiliana na majanga ya aina hiyo yatakapotokea siku za mbele.

“Iko haja ya kuimarisha mifumo yetu ya afya ili tuweze kujitayarisha kukabiliana na maradhi ya mlipuko kama COVID 19 na lazima tufahamu kuwa COVID siyo ya kwanza na wala siyo ya mwisho kuna milipuko itakuja tujiandae, Covid.” Amesititiza

Chanzo: www.tanzaniaweb.live