Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yahimiza watumishi kupima afya

03adc1aaaa8861bf12a0f45b484888f6.jpeg Serikali yahimiza watumishi kupima afya

Tue, 4 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imewataka watumishi wa umma kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua hali zao kama Mwongozo wa Kudhibiti Virusi vya Ukimwi (VVU), Ukimwi na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza Mahala pa Kazi wa Mwaka 2014 unavyowataka.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Hezron Nonga, alitoa mwito huo wakati akifungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Alisema upimaji wa afya kwa watumishi wa umma kwa mujibu wa mwongozo huo wa mwaka 2014, ni jambo la lazima na si hiari.

Alisema kutokana na hali hiyo, watumishi wa umma wanatakiwa kupima afya zao ili kubaini matatizo waliyo nayo na kuwashirikisha waajiri wao ili kupata msaada.

“Kupima afya ni jambo la lazima na muhimu kwa mtumishi kwani kutasaidia hata kuongeza tija katika taasisi baada ya kila mtumishi kutambua hali ya afya yake,” alisema.

Alisema kutambua afya za wafanyakazi kutamwezesha mwajiri kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu mbalimbali.

“Kama mtumishi atakuwa na afya njema, basi atasaidia kuongeza uzalishaji katika taasisi, hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa mwongozo huo wa kudhibiti VVU, Ukimwi, pamoja na magonjwa sugu yasiyoambukiza, ” alisema.

Kadhalika alisema kuwa mara baada ya mtumishi kupima afya yake na kubainika kuwa ana matatizo kiafya zipo stahiki ambazo anatakiwa kupatiwa.

Profesa Nonga alisema mtumishi ambaye atabainika baada ya vipimo kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi taratibu zinamtaka mwajiri wake kumpatia Sh 100,000 kila mwezi.

Alisema pamoja na kuwataka wafanyakazi kupima afya zao, pia wanatakiwa kutambua namna ya kuishi hasa katika kuzingatia masuala ya ulaji wa vyakula, unywaji wa pombe, ufutaji wa sigara.

“Wafanyakazi wanatakiwa pia kufanya mazoezi ili kuondokana na tatizo la uzito uliopitiza pamoja na msongo wa mawazo,” alisema.

Mratibu wa Ukimwi, VVU na magonjwa sugu yasiyoambukiza mahala pa kazi (Sekta ya Mifugo), Rachel Maliselo, alisema lengo ni kutoa fursa kwa wafanyakazi kupima afya zao kwa mujibu wa mwongozo huo.

“Wafanyakazi wetu wamefurahi sana kupata fursa hii kwani inawapa nafasi ya kutambua afya zao na kufanya kazi zao kwa bidii na kuongeza tija katika maeneo yaoa ya kazi,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz