Dar es Salaam. Katika kuongeza ufanisi na kasi ya upimaji Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini, Serikali imesema imeboresha mradi wa utoaji mafunzo kwa wataalamu wa maabara kupitia njia ya mtandao.
Mafunzo hayo ambayo yalianza rasmi 2016 yamewezesha kuvifikia vituo 21 vya afya katika mikoa minne ambako kasi ya maambukizi ni kubwa.
Akizungumza leo Jumanne Septemba 4, 2018 katika mafunzo yanayoendelea jijini hapa mkurugenzi wa uhakiki wa ubora wa huduma za afya wa Wizara ya Afya, Dk Mohamed Ally Mohamed amesema pamoja na kupunguza gharama mafunzo hayo yameongeza idadi ya wataalamu kwenye vituo vya afya hivi karibuni.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ambao si wa maabara ili waweze kufanya vipimo vya VVU kwa usahihi.
"Tunatoa mafunzo kwa wataalamu wa maabara wanaopima virusi vya Ukimwi kwa sababu tunatakiwa tupime watu wengi na kwa muda mfupi," amesema.
Kwa sasa mafunzo hayo yameanza kufanyika katika mikoa minne ikiwamo Mbeya, Njombe, Iringa na Shinyanga ili kuwafikia watoa huduma 10,000.
"Tumeweza kuwafikia watu wengi kwa mara moja na kwa gharama chache kupitia mtandao wa simu wa TTCL na mitandao mingine na hii imepunguza safari ili wahudumu wabaki kwenye vituo vyao," amesema.
Mkuu wa Mradi wa Maabara wa taasisi ya kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS), Charles Kagoma amesema kupitia mtandao wameweza kuwafundisha wataalamu hasa maeneo ya vijijini bila kuathiri huduma za afya.
"Teknolojia hii inatumika kuboresha huduma ya upimaji VVU lakini kwa uhaba wa wataalamu wa maabara tunataka upimaji ufanyike na wataalamu wengine wa afya ambao si wa maabara ili waweze kupima kwa usahihi," amesema.
Amesema mpango huo ni wa dunia nzima ambao unalenga kuongeza idadi ya watoa huduma za upimaji kwa njia za vipimo vya kawaida.
"Kasi ya upimaji inaongezeka nchi nzima na hii unaweza kuifanikisha ukiwa na watoa huduma wengi wanaoweza kupima kwa usahihi na majibu yakawa ya uhakika,"amesema.
Mradi huo unaoendeshwa na THPS, Health Links Initiatives (HLI) pamoja na Wizara ya Afya utawezesha kutoa mafunzo kwa vituo vya afya zaidi ya 50 nchi nzima kwa mtandao.