Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yabainisha masharti kupata leseni ya udaktari

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wahitimu wote wa masomo ya udaktari na uuguzi watalazimika kufanya mtihani mmoja wa kupimwa uwezo wao ili kukidhi vigezo vya kupata leseni ya kutoa huduma za afya.

Mtihani huo ni kwa mujibu wa sheria namba 11 ya mwaka 2017 iitwayo (The Medical Dental and Allied Health Professionals Act namba 11 ya mwaka 2017).

Hayo yamebainishwa Ijumaa Februari 22, 2019 na Mganga mkuu wa Serikali, Profesa Profesa Muhammad Bakari Kambi alipokuwa akifunga mkutano wa siku mbili wa wadau wa afya kutoka vyuo vyote vya afya Tanzania.

Alisema mtihani huo hautaishia kwa wataalamu wa afya wa fani ya udaktari na uuguzi peke yao, bali utaendelea kwenye kada zote.

Pia, mkutano huo ulikuwa na wawakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Madaktari Nchini (MCT) ikiwa ni kuelekea kuanzishwa kwa mtalaa linganifu wa mafunzo kwa wataalam wa afya, unaoendeshwa na mradi wa elimu kwa watoa huduma kwenye sekta ya afya Tanzania (THET).

Mganga mkuu alisema lengo la mtihani huo, utakaofanyika mara baada ya kumaliza shahada ni kupima uwezo wa watoa huduma za afya.

Profesa Kambi aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Zainab Chaula alisema ili sheria hiyo itekelezeke ilikuwa inahitaji kanuni nyingi zinazotengenezwa ambazo mojawapo ni pamoja na kufanya mtihani kwa wahitimu wa fani hiyo.

Alifafanua kuwa sheria hiyo inasema “Mtu hawezi kusajiliwa chini ya sheria hadi akidhi vigezo ikiwamo kufaulu mtihani huo utakaotolewa na Baraza.”

“Mtihani huu unafanyika mara baada ya kumaliza shahada, zamani kila chuo kilikuwa na mtihani wake, lakini kupitia sheria hii baraza litaandaa mtihani mmoja ambao utafanywa na wahitimu wote wa ndani na wa nje ya nchi,” alisema.

“Wahitimu kutoka vyuo vyote vya afya wataufanya ili kupima uwezo wao wa kutoa huduma za afya,” alisema.

Mganga mkuu huyo alisema haijalishi wanafunzi wametoka chuo gani badala yake ni kuzingatia ubora.

“Moja ya mikakati yetu kama wizara ni kuhakikisha tunaboresha utoaji huduma za afya na ili uboreshe lazima wataalamu wapate vigezo ambavyo sisi tunavihitaji ndani ya nchi,” alisema Profesa kambi.



Chanzo: mwananchi.co.tz