Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaanza ukaguzi ili kudhibiti upotevu wa dawa mahospilini

Msd.png Serikali kuanza ukaguzi ili kudhibiti upotevu wa dawa mahospilini

Tue, 28 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amesema uhaba wa dawa katika hospitali za umma nchini, unatokana na upotevu wa dawa unaofanywa na watumishi wasiyo waadilifu.

Amesema ili kudhibiti hali hiyo, serikali imeanzisha mfumo mpya wa kukusanya taarifa zote katika kila idara kwa lengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa watumishi wa wizara hiyo.

Waziri Dorothy aliyaeleza hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao cha wataalamu na wadau wa masuala ya ugavi wa dawa nchini na kuwataka kuweka mpango mkakati wa kutunza taarifa ili kufahamu dawa zinapopotelea.

"Suala la upotevu wa dawa linafanywa na watu wachache ambao kwa mbinu zao wanaweza kuleta uharibifu mkubwa sana, tumebaini pamoja na serikali kuongeza bajeti ya dawa, pamoja na kuagiza dawa moja kwa moja kutoka viwandani tushushe bei pamoja na kusambaza dawa zifike kwenye vituo, kama hatujaziba kule zinapotumika zitumike vizuri tutapata uharibifu na kutokutesheleza kwa mahitaji haya," alisema Dk. Dorothy.

Alisema suala hilo siyo usimamizi mbovu bali uwajibikaji na ufuatiliaji wa rasilimali za umma unaofanywa na watendaji wasiyo waadilifu.

"Unaweza usiwe mdokozi, lakini unanunua dawa nje ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kule gharama ni kubwa na mtaji ukaisha, lakini ukanunua MSD lakini dawa zisifike kituoni na zikafika kituoni zisifike kwa mlaji ambaye ni mgonjwa na ndio maana hizi takwimu tukiziangalia hatuzioni kwenye taarifa zetu," alisema Dk. Dorothy.

Alisema matokeo ya mfumo wa ufuatiliaji wameanza kuyaona, ukilinganisha na miezi mitano iliyopita kabla ya kuwapo kulikuwa na upotevu mkubwa wa dawa."Waliofanya ufuatiliaji na waliyoyakuta kule ni makubwa, hakuna upotevu wa dawa na hakuna bajeti iliyoongezwa, tutakuja kuwaeleza kuhusiana na hili ila mfumo huu umesaidia kudhibiti upotevu kwa asilimia kubwa," alisema.

Akizungumzia maeneo 16 ya mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya yaliyofanyiwa ufuatiliaji katika hospitali za rufani za mikoa na thamani ya upotevu wa fedha kwa kila eneo ambao taarifa zake zilitolewa Machi 3, mwaka huu alisema ulifanyika kwa miezi 18 na idadi ya bidhaa 25-20.

Alisema walibaini ankara ambazo hazikuonekana kwenye hospitali za rufani za mikoa ni Sh. bilioni 11 na bidhaa zilizo na ushahidi wa kuwa zimetoka bohari kwenda kutumika ni za Sh. bilioni 3.2

Waziri huyo alitaja pia walibaini bidhaa zilizopelekwa kituo kingine hazijawahi kufika ni za Sh. milioni 354.7, bidhaa zilizofika kwenye idara au kitengo kutofika kwa wagonjwa Sh. bilioni 2.4 na bidhaa ambazo zilinunuliwa kwa washirika bila kibali cha MSD Sh. bilioni 5.6.

Nyingine ni bidhaa zilizonunuliwa MSD na washitiri teule Sh. bilioni 1.12, bidhaa zilizonunuliwa kwa washitiri kinyume na mkataba Sh. milioni 640, bidhaa zilizonunuliwa bila kuidhinishwa na kamati ya Dawa na Tiba Sh. Bilioni 1.9 na bidhaa ambazo wateja wanachama wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) walikosa Sh. bilioni 6.1

Naye Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, alisema nchini kuna viwanda 18 vilivyopo katika hatua mbalimbali, vingine vimeanza uzalishaji kwa lengo la kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi kutoka asilimia 88 ya sasa hadi kufika chini ya asilimia 50 mwaka 2030.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live