RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wauguzi ili watimize majukumu yao vizuri na kwa usalama.
Alieleza hayo jana kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akizungumzia sherehe za Siku ya Wauguzi Duniani.
“Nawatakia heri Wauguzi wote katika kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani. Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu katika jamii. Nawaahidi kuwa tutaendelea kuboresha mazingira na maslahi yenu ya kazi ili mtimize majukumu yenu vizuri na kwa usalama. Chapeni kazi, tunawategemea”aliandika Rais Samia.
Siku ya kimataifa ya wauguzi duniani inaadhimishwa kila mwaka Mei 12 kuthamini juhudi za wauguzi katika kuhudumia wagonjwa ,pia siku hiyo ni kumbukumbu ya mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa Florence Nightingale.
Baraza la Kimataifa la Wauguzi (ICN) limekuwa ikisherehekea siku hiyo tangu mwaka 1965.
Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu (pichani) jana alisema serikali ku endelea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa wauguzi.
Aliyasema hayo mkoani Manyara wakati maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Ummy alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilijenga na kukarabati miundombinu ya utoaji wa huduma za afya na kuweka vifaa tiba na kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuongeza wahudumu wa afya.
Alisema serikali imetoa ajira mbadala za wauguzi 2,726 na kwamba wanaoomba ajira ni wengi.
Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuacha kuwanyima wauguzi fursa ya kwenda kuongeza ujuzi.
Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya alisema ni vyema serikali kuendelea kuwekeza kwenye taaluma hiyo ili iwe madhubuti na yenye weledi.
Baluhya aliiomba serikali iendelee kuitetea na kuisimamia taaluma ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekelezwa yale ambayo yapo kwenye misingi ya taaluma hiyo.
Baluhya alimuomba Ummy awasaidie kupitia mamlaka za halmashauri wanapopata majina ya wauguzi walioamua kujiunga na chama cha wauguzi kusiwe na vikwazo vya kukatwa ada kwenye mishahara.
Juzi Baluhya alisema serikali imeiboresha sekta ya afya lakini wanahitaji ajira za wauguzi na wakunga.
Baluhya alisema hayo wilayani Babati katika kongamano la wauguzi kujiandaa kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani.
Imeandikwa na Mariam Juma na Theddy Chale, Babati