Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaagiza TMDA, ZMDA wasimamie udhibiti, tafiti

5fc65396f46ba4786be7fd47fc12a073.png Serikali yaagiza TMDA, ZMDA wasimamie udhibiti, tafiti

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imezitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TMDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZMDA) kuhakikisha zinasimamia kikamilifu suala la udhibiti na tafiti za dawa na vipimo ili kuleta majibu yenye tija yatakayolisaidia taifa kupiga hatua kimaendeleo.

Aidha, imevitaka vyuo na taasisi zinazofanya utafiti huo, kushirikiana na mamlaka hizo ili kufanya utafiti wenye viwango bora sanjari na kutoa fursa kwa watafiti wanaochipukia hatua ambayo pamoja na mambo mengine, itawasaidia kuwa watafiti bora.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi, aliyoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mradi ujulikanao kama Ascend ambao pamoja na mambo, mengine umelenga kuzijengea uwezo mamlaka na taasisi hizo katika eneo la udhibiti na tafiti za dawa na vipimo.

Alisema kimsingi kama mamlaka hizo zitasimamia majukumu yao katika usimamizi wa tafiti na vipimo, zitasaidia kuleta majawabu sahihi ya vipimo hivyo, kutibu kwa haraka hali itakayopunguza changamoto zinazowakabili wananchi.

"Aidha TMDA na ZMDA kwa pamoja zinapapswa kuhakikisha zinapunguza gharama za mafunzo kwa watafiti vijana wanaofika katika ofisi zenu kutaka kufanya utafiti wao, mkihakikisha pia mnawasimamia vizuri," alisema Profesa Makubi.

Alisema serikali inaunga mkono mradi huo kwa kuwa utaleta matokeo chanya katika sekta ya afya ukisaidia kuongeza idadi ya watafiti nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, alisema mradi huo wa miaka miwili na nusu unaofadhiliwa na umoja wa nchi za Ulaya, umelenga kudhibiti mifumo ya dawa na kuimarisha utafiti.

Alisema Ascend licha ya kuzihusisha taasisi nchini, pia unazihusisha taasisi zilizopo nje ya nchi, hasa katika eneo la kuzijengea uwezo wa mafunzo taasisi za hapa nchini.

Alizitaja taasisi zinazohusika katika mradi huo kuwa ni pamoja na Kituo cha Utafiti cha Kilimanjaro (KCRI), Chuo cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHA'S), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Afya Zanzibar (ZAHRI), UStAN, ZFDA, na TMDA.

Chanzo: habarileo.co.tz