Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yazungumzia homa ya Corona, yatoa wito kwa Watanzania

93394 Pic+corona Serikali ya Tanzania yazungumzia homa ya Corona, yatoa wito kwa Watanzania

Wed, 29 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mpaka sasa hakuna Mtanzania anayeishi nchini China ambaye amekumbwa na ugonjwa wa homa ya Corona.

Akitoa taarifa ya ugonjwa huo jana Jumatatu Januari 27,2020, Profesa Kabudi amesema hadi sasa Watanzania wote wanaoishi China katika Jimbo la Wuhan hakuna hata mmoja wao ambaye amepatikana na ugonjwa huo.

Alisema Tanzania ina wanafunzi takriban 4,000 wanaosoma China na katika mji wa Wuhan ambao umekumbwa na mlipuko wa virusi vya corona kuna wanafunzi 400 lakini hakuna Mtanzania ambaye amekumbwa na ugonjwa huo.

“Leo (jana) nimekuwa na mazungumzo na Balozi wa Tanzania anayetuwakilisha China, ambaye amenihakikishia hadi sasa Watanzania wote walioko huko China na katika Jimbo la Wuhan hakuna hata mmoja wao ambaye amepatikana na hiyo homa,” alisema Profesa Kabudi

“Taarifa mpaka leo (jana) nilipozungumza na Balozi wa China, Balozi Mbelwa Kairuki mpaka sasa hakuna Mtanzania ambaye amekumbwa na homa hiyo ya Corona” alisema

Profesa Kabudi aliwataka Watanzania kuwa watulivu na wapende kuwa na subira ya kupata taarifa kutoka kwenye vyombo husika badala ya kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii au uvumi.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
 “Wale wote wenye ndugu zao China ambao ni Watanzania, tunataka kuwahakikishia kwamba taarifa zozote tukizipata tutawapa, kwa hiyo watulie na tukipata taarifa zozote kuhusu Mtanzania kupata homa hiyo hatutasita kuiarifu familia na jamaa yake, hilo ndio ombi langu kwa Watanzania wote” alisema

Virusi hivyo vya homa ya corona vimeibuka tangu mwishoni mwa Desemba 2019 na husababisha mafua makali huku dalili zikielezwa kuwa ni mwili kupanda joto.

Taarifa zinasema kuwa tayari watu zaidi ya 50 wameshapoteza maisha kutokana na virusi hivyo vipya, huku vifo vitatu vikiripotiwa nje ya Wuhan huku walioambukizwa wakifikia 1,300 na tayari umesambaa katika nchi za Ufaransa, Marekani, Thailand, Japan, Taiwan, Korea Kusini na Macau.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz