Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yatoa somo kwa watumishi kuhusu dawa za umma

Wed, 16 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Dk Faustine Ndugulile amewataka watumishi wa afya nchini kuwa waadilifu katika utendaji wao hasa katika matumizi ya dawa za Serikali.

Amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kisheria watumishi watakaobainika kuiba dawa za Serikali zinazopelekwa katika vituo mbalimbali vya afya.

Dk Ndugulile ametoa rai hiyo leo Jumanne  Oktoba 15, 2019 katika ufunguzi wa mkutano ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Idadi ya watu (UNFPA) unaojadili mnyororo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba jijini Dar es Salaam.

“Hivi sasa hatua ambazo tunachukua ili kudhibiti wizi wa dawa ni kuzipeleka kwenye kituo cha afya hadi mlangoni lakini pia hazipokelewi kienyeji bali kuna kamati maalumu za kupokea dawa hizo,” amesema.

Aidha ameonya baadhi ya wamiliki wa maduka binafsi ya dawa kuacha kuuza dawa za Serikali na kwamba watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kama wahujumu uchumi.

“Kwa hiyo, hata wananchi wanatakiwa kutambua hili, kwamba kuna baadhi ya watumishi wanaiba dawa na kuzipeleka kwenye maduka binafsi ya dawa hivyo mwananchi yeyote atakayeuziwa dawa yenye nembo ya Serikali (MSD) au ambayo haina kifungashio kabisa atoe taarifa ili tuweze kuchukua hatua kwa sababu ni dawa yetu,” amesema.

Pia Soma

Advertisement

Hata hivyo, amesema tofauti na zamani hivi sasa Serikali imefanikiwa kudhibiti upotevu wa dawa na kwamba malalamiko ya wananchi kukosa dawa yamepungua.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo  Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Jackline Mahon amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha huduma za afya kwa Watanzania zinaboreshwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz