Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yasema Dengue imeua wanne, wagonjwa 4,320

Video Archive
Fri, 21 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati homa ya dengue ikiwa gumzo kila kona, Serikali ya Tanzania imesema watu wanne wamefariki dunia kuanzia Januari hadi Juni, 2019 kutokana na ugonjwa huo.

Pia, imetangaza kutoa vipimo bure kwenye vituo vya kutoa huduma za afya vya umma.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Juni 21, 2019 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akisoma kauli ya Serikali kuhusu ugonjwa huo, kueleza changamoto tatu za kuudhibiti.

Amesema kuanzia Januari, 2019 wagonjwa 4,320 na vifo vinne vimeripotiwa huku Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa 4,029 na vifo vitatu.

“Mkoa wa Dodoma wagonjwa walikuwa watatu na kifo kimoja. Tanga wagonjwa 207, Pwani 57, Morogoro 16, Arusha wagonjwa watatu, Singida wawili, Kagera pia wawili. Vifo vimetokea katika hospitali ya rufaa Dodoma na Dar es Salaam katika hospitali ya Hindu Mandal na Regency,” amesema Ummy.

Kuhusu changamoto, Ummy amesema ya kwanza ni gharama za kupima, “Ingawa Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imenunua vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na kuviuza kwa bei nafuu ikilinganishwa na gharama inayotozwa kwenye baadhi ya hospitali binafsi, bado wananchi wanashindwa kumudu gharama za uchangiaji matibabu ya ugonjwa huu.”

Pia Soma

“Pili, jamii haijaweza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni ya usafi wa mazingira ambayo ni njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mtu na tatu ni watoa huduma za afya kutofuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa huu.”

Wizara ya Afya kununua lita 60,000 za viuadudu kuangamiza mazalia ya mbu wapevu na viluwiluwi na kusambaza katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Kigoma, Lindi na Mtwara ni moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti ugonjwa huo.

“Serikali itaboresha matibabu kwa wagonjwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa dawa za kutosha na pia itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa afya sambamba na kuboresha mifumo ya ukusanyaji takwimu,” amesema Ummy.

Dengue ni nini

Ugonjwa wa dengue huenezwa na mbu aina ya Aedesambae, mbu mweusi mweye madoa meupe ya kung’aa  ambaye hupendelea kuuma hasa wakati wa asubuhi, mchana na jioni. Dalili za ugonjwa huo ni  homa ya ghafla, kuumwa na kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu.

Chanzo: mwananchi.co.tz