Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yaelezea jinsi ilivyotumia mabilioni kujenga na kukarabati vituo afya

Tue, 18 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imejenga, imekarabati na kupanua vituo vya afya, hospitali na zahanati 352 nchini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18, Bunge limeelezwa leo Jumanne Juni 18,2019.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri ofisi ya Rais Tamisemi, Josephat Kandenge wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) Emmanuel Mwakasaka.

Mbunge huyo ameuliza Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha katika bajeti ili kuzisaidia halmashauri kujenga hospitali na vituo vya afya badala ya kuziachia halmashauri.

Naibu waziri amesema katika orodha hiyo, hospitali zilikuwa tisa, vituo vya afya 304 na zahanati 39 ambapo zilitumia Sh184.67 bilioni lakini kwa mwaka 2018/19 Serikali ilitenga Sh100.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za halmashauri.

Aidha naibu waziri amesema kwa mwaka 2019/20, Serikali imetenga Sh10.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo 52 vya afya na Sh46.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 27 za halmashauri.

Chanzo: mwananchi.co.tz