Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yaeleza hatua uboreshaji wa huduma za afya

69616 Afya+pic

Sat, 3 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeahidi kushughulikia kero mbalimbali zinazoendelea katika huduma za afya hususani kwa wakazi wa maeneo ya vijijini kupitia utekelezaji wa miradi chini ya Rais John Magufuli.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Dk Ntuli Kapologwe amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali imetoa ajira 12,450 kwa watumishi watakaotoa huduma katika ngazi mbalimbali.

Dk Kapologwe amesema ajira hizo zilitolewa sanjari na ujenzi wa vituo 470 vya afya katika ngazi ya kata, hatua iliyowezesha kufikia idadi ya kata 700 kati ya 4,420 zinazotoa huduma za afya.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 2, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Taasisi inayoendesha Kongamano la Afya Tanzania (THS).

“Tumejenga vituo vya afya 470 ndani ya miaka miwili, sasa ukishajenga vituo utahitaji na watumishi kwa wingi, changamoto ipo lakini tunashukuru tumeweza kuajiri watu 12,450 wa kada mbalimbali kati ya mwaka 2017 mwishoni hadi sasa (Agosti 2019).”

“Upungufu wa watoa huduma upo karibu kwenye asilimia 50 lakini upungufu huo umeongezeka baada ya kuongezeka kwa idadi ya vituo vya afya,” amesema.

Pia Soma

Uzinduzi wa bodi hiyo unafanyika ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa Kongamano la sita mjini  Dodoma likikutanisha wadau zaidi ya 600 wa sekta hiyo kujadili ajenda sita, ikiwemo utoaji wa huduma za afya, uongozi na utawala, matumizi ya Tehama na uchangiaji wa huduma.

THS ilianzishwa mwaka 2014 chini ya mwamvuli wa sekta binafsi na wanataaluma wa huduma za afya ili kukutanisha wadau wa sekta hiyo kupitia kongamano kwa lengo la kujadili changamoto na mafanikio, fursa na mbinu mpya zinazochochea ubora na utosherevu wa huduma hiyo kwa kila Mtanzania.

Rais wa THS, Dk Omary Chillo amesema mchango unaopatikana kupitia kongamano hilo umekuwa na mafanikio mbalimbali yaliyoonyesha matokeo chanya katika huduma za afya ikiwamo kusogeza huduma na uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa vipimo, tiba na kinga za magonjwa yasiyoambukizwa.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz