Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yaandaa maeneo ya matibabu virusi vya Corona

92950 Pic+virusi Serikali ya Tanzania yaandaa maeneo ya matibabu virusi vya Corona

Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imeandaa maeneo maalum ya matibabu ikiwa watabainika wagonjwa watakaopata maambukizi ya virusi hatari vya corona vilivyoua watu 17 nchini China hadi jana Alhamisi Januari 23, 2020.

Virusi hivyo vinavyofanana na ugonjwa wa SARS (ugonjwa unaoathiri mfumo wa hewa) vimezua taharuki duniani na leo Ijumaa Januari 24, 2020 Wizara ya Afya ya Tanzania imeeleza mkakati wake kuhusu ugonjwa huo.

Tayari virusi hivyo vimeshaathiri watu zaidi ya 440 nchini China na wengi wao wakitoka Wuhan, AFP imeripoti. Li Bin wa Kamisheni ya Afya ya Taifa ya China alikaririwa na AFP akisema watu 1,394 walikuwa wakiendelea kuangaliwa na wauguzi.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Januari 24, 2020 na mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini- afya, Gerald Chami inaeleza kuwa hadi sasa Tanzania hakuna aliyepata ugonjwa huo.

Chami amesema wameandaa maeneo maalum ya matibabu kwa wagonjwa watakaogua nchini na kuandaa vifaa vya kutolea huduma vikiwemo vifaa kinga.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mafua makali uliozikumba nchi za China, Thailand, Japan, Korea ya Kusini na Marekani ulianza mwanzoni mwa Desemba 2019.

Pia Soma

Advertisement
Takwimu za mlipuko huo zinaonyesha kuwa hadi kufikia Januari 22, 2020 watu wapatao 560 wameathirika huku vifo vikiwa 17 ambapo nchi ya China imethibitisha wagonjwa 550 vifo 17.

Chami amesema kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo hasa kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na nchi za Bara la Asia ikiwemo China, Tanzania pia ipo katika hatari ya ugonjwa huo.

“Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi wote hususani ambao wanasafiri kwenda kwenye mataifa yaliyoathirika na mlipuko wa ugonjwa huo na wale wanaopokea wageni kutoka katika nchi hizo,” amesema Chami.

Amesema Wizara imechukua hatua kukabiliana na tishio la ugonjwa huo ikiwemo kuendelea kuimarisha ufutiliaji kwenye vituo vyote vya huduma pamoja na uchunguzi wa wasafiri kutoka nje ya nchi, mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandari.

“Wizara inachukua na kupima sampuli kutoka maeneo ya ufuatiliaji na yeyote anayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo kupitia maabara ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za ugonjwa huu wa viongozi wa afya katika ngazi zote kuanzia waganga wakuu wa mikoa na halmashauri zote nchini, ikiwemo mafunzo kwa watoa huduma,” amesema Chami.

Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia kanuni za afya kwa  kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua mwenye,  historia ya kusafiri katika nchi zilizokumbwa na mlipuko au mwenye dalili zilizotajwa .

Fanya haya kuepuka virusi vya Corona

 

  1. Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo uliyovaa sehemu za mikono.
 

  1. Epuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa.
 

  1. Zingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
 

  1. Kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili zilizoainishwa.
 

  1. Kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz